Saturday, 19 October 2019

RC MNYETI AWAFAGILIA DC MAGESSA NA DED KAMBONA


 Mkuu wa Mkoa wa Manyara,  Alexander Pastory Mnyeti, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kiteto katika Mji mdogo wa Kibaya. 
 Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mhandisi Tumaini Chaula akimsikiliza Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilayaya Kiteto, Tamimu Kambona akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti.

MKUU wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amesema Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mhandisi Tumaini Magessa anaongoza kwa utendaji mzuri na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona ndiye Mkurugenzi anayeongoza Mkoani humo kwa uchapakazi ikiwemo kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo. 

Mnyeti aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Kibaya kwenye ziara yake ya siku tano wilayani Kiteto. Alisema mkuu wa wilaya ya Kiteto mhandisi Magessa ni mchapakazi mzuri katika mkoa huo akishirikiana na Mkurugenzi wake Kambona hivyo wapewe ushirikiano. 

Alisema japokuwa baadhi ya watu wanamlalamikia mkuu huyo wa wilaya lakini maeneo mengine wanatamani kuwa na mkuu wa wilaya kama mhandisi Magessa. 

"Pamoja na changamoto zilizopo hapa Kiteto ningekuwa natoa maksi ningewapa asilimia 95 kati ya 100 na hiyo ni kutokana na utendaji mzuri wa viongozi wa Kiteto wakiongozwa na Magessa na Kambona," alisema Mnyeti na kuongeza:

"Naomba mnisikilize vizuri mimi ndiye mkuu wa mkoa wenu nawahakikishia kuwa halmashauri inayofanywa vizuri kwenye mambo mengi katika mkoa huu ni Kiteto."

Alisema ubora wao unatokana na kusimamia vyema miradi mbalimbali ya maendeleo usimamizi mzuri hivyo wanapaswa kupongezwa kutokana na hayo. Alisema viongozi wengine wa wilaya na halmashauri za mkoa wa Manyara wanapaswa kwenda Kiteto ili wakajifunze namna ya kusimamia miradi yao ya maendeleo. 

"Ukifika Kiteto unakuta miradi bora yenye kiwango ambayo imejengwa kwa fedha pungufu na huwezi kuacha kuizindua kama baadhi ya maeneo ambapo nimepita na kukuta uchakachuaji," alisema Mnyeti. 

Alisema amefika Kiteto ameshuhudia ujenzi wa baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo madarasa ambapo wamepatiwa fedha za ujenzi wa madarasa matatu lakini wao kwa fedha hizo hizo wamejenga madarasa manne yenye ubora. 

"Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wengine waliopo katika mkoa wa Manyara wanapaswa kuja Kiteto kuiga maendeleo mazuri yanayofanyika hapa," alisema Mnyeti. 

Mkuu wa wilaya ya Kiteto, mhandisi Tumaini Magessa alishukuru kwa pongezi hizo na kuahidi hawatarudi nyuma katika kuhakikisha wanasimamia maendeleo kwa manufaa ya wananchi. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona alisema lengo lao ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inasimamiwa ipasavyo ili mwisho wa siku mwananchi afaidike. 

No comments:

Post a comment