Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa akisisitiza uhifadhi mzuri wa nyaraka alipotembelea maktaba ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam na kushuhudia baadhi ya watafiti wakipata huduma ya taarifa zitakazowawezesha kukamilisha tafiti zao.
IMEELEZWA kuwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere katika Maporomoko ya Mto Rufiji unaojulikana kama Julius Nyerere HydroPower Project ambao Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa vitendo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere mnamo mwaka 1975.  
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa mara baada kufanya ziara ya kikazi Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam na kujionea kitabu cha Tanzania News Review cha mwaka 1977 kinachoainisha kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ndiye Muasisi wa mradi huo.
Dkt. Mwanjelwa amesema, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza masuala yenye maslahi kwa taifa yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere.
“Hakika ule usemi wa zidumu fikra za Mwalimu Nyerere umetekelezwa kwa vitendo na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Magufuli katika ujenzi wa mradi huu,” amefafanua Dkt. Mwanjelwa.
Aidha, Dkt Mwanjelwa ameitaka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuwa na utaratibu mzuri wa kuuhabarisha umma juu ya taarifa muhimu za kihistoria ambazo si za siri ili watanzania wajue maamuzi mbalimbali ya kizalendo yaliyofanywa na viongozi wao kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi amemhakikishia Dkt. Mwanjelwa kuwa Idara yake itaendelea kutunza vizuri na kwa uadilifu mkubwa nyaraka muhimu za nchi za kabla na baada ya uhuru kwani nyaraka hizo ni rejea muhimu katika utendaji kazi wa Serikali.
Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere katika Maporomoko ya Mto Rufiji unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022 na utakuwa ukifua megawati 2,115 kwa siku.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: