Wakulima wa Zao la Korosho Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kujiepusha na walanguzi wanaouza viutilifu kwa ajili ya kupulizia mikorosho msimu 2018/2019.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Homera ametoa angalizo hilo wakati wa mikutano ya hadhara aliyoifanya hii leo katika kata za Namiyungu,Namakambale,Nakapanya na Tinginya yenye lengo la kuhamasisha wakulima wa Korosho kutumia viuatilifu vinavyosambazwa na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).

Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa wapo wafanyabiashara wanawalangua wakulima wa Korosho kwa kuwauzia mfuko mmoja wa salfa wa kilo 25 kwa bei ya shilingi 50,000/= hadi 65,000/= jambo ambalo ni kinyume na bei elekezi ya Serikali ya Shikingi 32,000/= kwa mfuko mmoja ,huku wengine wakiwa wameichakachua salfa hiyo na kujaza unga wa muhogo.

Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Korosho Tawi la Tunduru Bi.Shauri Mokiwa  amewatoa hofu wakulima wa Korosho juu ya upatikanaji wa viuatilifu akisema kwamba Tunduru ina mgao wa kutosha wa kuweza kuwahidumia wakulima wote.

Afisa uhusiano wa Bodi ya Korosho Tanzania Bryson Mshana amesema ziara hiyo ya kutembelea maeneo yote yanayolima Korosho katika wilaya ya Tunduru inaratibiwa na CBT ikishirikiana na Serikali ngazi ya Wilaya,na inalenga kuwahamasisha wakulima kutumia viuatilifu vinavyosambazwa na Serikali.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: