Wednesday, 25 April 2018

TSHISHIMBI AKODIWA GARI MAALUM, APELEKWA MORO

KIUNGO wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, jana jioni alikodiwa gari maalum ambalo lilimpeleka mkoani Morogoro ambapo kikosi kizima cha timu hiyo kimeweka kambi mkoani humo.

Yanga ambayo Jumapili ya wiki hii itapambana na Simba, imeweka kambi Morogoro tangu juzi Jumatatu ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Tshishimbi ambaye amechelewa kujiunga na wenzake kutokana na awali kubaki jijini Dar kutokana na kusumbuliwa na majeraha, kwa sasa yupo fiti na kuna uwezekano Jumapili akacheza dhidi ya Simba.

Mtoa taarifa kutoka ndani ya Yanga ambaye hakupenda kuandikwa jina lake, ameliambia Championi Jumatano kuwa: “Wenzake waliobaki Dar walitangulia, lakini yeye kuna mambo alikuwa akiyaweka sawa na leo (jana Jumanne) tumemkodia gari limpeleke Morogoro aungane na wenzake. Alikuwa majeruhi lakini kwa sasa yupo fiti.”
Wakati Tshishimbi akiungana na wenzake jana, wachezaji wengine wa Yanga ambao hawakwenda na timu mkoani Mbeya ambao ni Hassan Kessy, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe na Andrew Vincent ‘Dante’, waliungana na wenzao juzi Jumatatu.

Ikumbukwe kuwa, Jumapili hii, Yanga itacheza na Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo katika kujiandaa na mchezo huo, timu hizo zote zimepiga kambi mkoani Morogoro.

No comments:

Post a comment