WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuwa wanazuia kuwepo kwa maandamano ili kutoruhusu watu wachache wanaotamani Tanzania wavurugane  na kuharibu taswira ya nchi.

Akizungumza jana katika harambee iliyoandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Masaka dayosisi ya Pare, wilayani Same, alisema kuwa katika maandamano hayo wapo watu watakaofanya vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na hata kufyatua risasi ili ionekane kwamba nchi inaua watu.

‘’Wapo wanaotamani tuvurugane na tunapowaeleza wananchi wanaweza kujiuliza kwanini tunazuia maandamano wakati wapo watu wanaofanya mazoezi na ni kwa sababu hatutaki kuruhusu watu watuburuge,’’ alisema Dk Mwigulu.

Alisema wapo watu wenye mitazamo mibaya zaidi ambao wataiba na pia wataandaliwa watu watakaofyatua risasi ili ionekane watu wameuawa katika maandamano.

Alisisitiza kuwa lengo la kuzuia maandamano ni baada ya kuangalia kwa jicho la tatu maandamano hayo hivyo raia na vyama vya siasa wawaelewe kwani hawana nia ya kuminya uhuru wao ambao upo kwa mujibu wa katiba.

‘’Tunaangalia sura ambayo adui anaweza kupitia, wasione majira haya ni ya kawaida kuna mahali tumegusa hivyo hawafurahi na ndio sababu haya mambo yanatokea hivyo tunaomba msichukulie kuwa ni vitu vyepesi vyepesi bali mpanue mitazamo yenu mnapoona masuala haya yanapojitokeza,’’ aliongeza.6
Share To:

msumbanews

Post A Comment: