Articles by "NHIF BIMA"
Showing posts with label NHIF BIMA. Show all posts


Na Grace Michael, Dodoma

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umepongezwa kwa mapinduzi chanya ya kihuduma ambapo kwa sasa inalipa madai kwa Watoa huduma kwa wakati ikilinganishwa na hapo awali.

Mbali na ulipaji wa madai, maboresho ya mifumo yaliyofanyika yamewezesha utatuaji wa changamoto na mawasiliano ya haraka kati ya Mfuko na Watoa huduma hatua inayorahisisha huduma kwa wanachama.

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Ibenzi Ernest wakati akizungumzia mashirikiano ya NHIF na Hospitali hiyo.

"NHIF kwa sasa inastahili kupongezwa kwa namna ilivyojipanga katika kutoa huduma na kwa upande wetu kama Watoa huduma tunalipwa kwa wakati na inapotokea changamoto tunakaa na kuitatua kwa haraka," amesema Dkt. Ibenzi.

Akizungumzia umuhimu wa Bima ya Afya, Dkt. Ibenzi amewataka wananchi kujiunga na NHIF kwa kuwa ndio mkombozi mkubwa katika suala la uhakika wa matibabu.

"Hakuna namna nyingine kwa sasa zaidi ya kupata huduma kupitia Bima ya Afya, wananchi wanaopata huduma kwa kadi wanakuwa na uhakika zaidi wa kupata huduma zote wanazozihitaji tofauti na wananchi wasikuwa na kadi hivyo niwaombe wananchi wajiunge ili wawe na uhakika wa kupata huduma bila kikwazo cha fedha," amesema Dkt. Ibenzi.

Kwa upande wa huduma Hospitalini hapo, amesema Serikali imewekeza vya kutosha katika maeneo yote hivyo ameweka wazi kuwa kwa sasa wana jukumu la kuwahudumia wananchi kwa utaalam na weledi zaidi.

Kwa upande wa wanachama waliokuwa wakipata huduma, wamesema kwa sasa wanapata huduma zote wanazozihitaji na wameahidi kuulinda Mfuko ili uendelee kuwa imara na uhudumie wananchi wengi zaidi.

Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge Sasa

 


Na WAF, DODOMA 

Serikali imesema huduma za afya ya akili zimeshajumuishwa kwenye vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na hivyo wananchi wanaonufaika na bima wanaweza kupata matibabu hayo kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu uliopo.

Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, huduma za afya ya akili, ushauri nasaha, pamoja na huduma za kibingwa kama vile utengamao, zote zimetajwa kama huduma muhimu kwenye Mwongozo wa Matibabu (Standard Treatment Guideline – STG) na zinagharamiwa na NHIF

“Huduma hizi zinalipiwa kwa kuzingatia aina ya dawa na ngazi ya kituo cha huduma, kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu wa Taifa,” amefafanua Naibu Waziri  Dkt. Mollel.

Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa huduma za afya ya akili zinapewa uzito sawa na huduma nyingine za msingi, na kuimarisha upatikanaji wake kupitia mifumo ya bima ya afya kwa wote.

 

WAKATI Mfuko wa bima ya afya ukijivunia mafanikio makubwa ya Mfuko chini ya uongozi wa awamu ya sita, kwa kuongeza mapato na wigo wa kutoa huduma, pia umefanikiwa kuokoa zaidi ya bilioni 22 zilizotokana na udanganyifu wa utoaji huduma ya afya kupitia vituo vya afya huku ikivifungia vituo vya afya 11 nchini kutokana na udanganyifu huo.

Hayo yameelezwa leo Machi10 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa bima ya afya nchini, Dkt. Irene Isaka alipokuwa akielezea mafanikio ya utoaji huduma ya Mfuko huo katika uongozi wa awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Irene amesema ndani ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita, jumla ya matukio 229 ya udanganyifu yanaendelea kufanyiwa uchunguzi katika ngazi mbalimbali za kisheria nchini kutokana na udanganyifu huo huku kadi 13,000 zikiwa zimefungiwa kupata huduma ya afya kote nchini.

Hata hivyo amesema mafanikio yote hayo yametokana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ambayo  inatumiwa na Mfuko huo katika awamu ya sita na kuondokana na mifumo wa kawaida.

Amesema katika kipindi hicho, watumishi 39 wameripotiwa kuhusika kwenye udanganyifu na walioonekana kuhusika moja kwa moja wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Dkt. Irene ametaja mafanikio mengine ya Mfuko huo ni pamoja na kuwa na ziada ya bilioni 95 za mapato hadi Disemba 2024. dhidi ya  nakisi ya bilioni 120 hapo awali hayo ni mafaniko ambayo yanatokana na kupunguzwa kwa gharama za uendeshaji, kubana matumizi na kukabiliana na udanganyifu.

“Napenda kuwaeleza tu kwamba hapo mwanzo Mfuko ulitetereka ulikuwa na uwezo wa kujiendesha kwa kipindi cha miezi 6 tu jambo ambalo ni hatari lakini hivi sasa Mfuko uwezo wa Mfuko umeboreka na unaweza kujiendesha kwa mwaka mmoja na miezi miwili  na tunataka kufikia uwezo wa kujiendesha miaka miwili kwa mujibu wa viwango vya kimataifa amesema na kuongeza:

“ Tumekuwa tukitumia mfumo wa kisasa wa kidijitali wa mawasiliano, yaani online system ambayo ni mfumo tunaotumia kufuatilia madai ya wabia na wagonjwa, mfumo huu umekuwa ukisaidia kuchakata madai na kuondoa udanganyifu, mfano unaumwa malaria lakini kituo cha afya umeandikiwa antibiotic mfumo unakataa kwa kuwa unatambua, mgonjwa wa malaria anatakiwa kunywa dawa gani,”anasema.

Amesema kwa kipindi cha miezi sita, Mfuko huo umefanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 384.20 na kusajili wanachama wapya 284,543 kipindi cha miezi sita. “ hii imesaidia kuongeza makusanyo hadi kufikia trilioni 2.3 katika kipindi cha uongozi wa awamu ya sita ambapo kati ya fedha hizo asilimia 92 zinatokana na makusanyo ya michango, asilimia 7 mapato ya uwekezaji na asimilia 1 vyanzo vingine.

Pia amesema ulipaji wa madai
 kwa vituo  vinavyotoa huduma kwa wanachama umeongezeka na hivyo kuongeza ubora wa huduma katika vituo hivyo vinavyotumia huduma ya NHIF kutokana na pato linalotoka katika Mfuko huo kuongezeka na kulipa kwa wakati tofauti na hapo mwanzo.

“ Tumeweza kulipa hospitali na vituo vya afya madai ya zaidi ya trilioni 2.29 ambayo ni sawa na asilimia 37 kwa hospitali za Serikali, asilimia 28 kwa hospitali za mashirika ya dini na asimilia 35 kwa hospitali binafsi,”amesema.

Amesema huduma za wazee yaani wastaafu zimeendelea kutolewa ambapo kwa kipindi cha mwaka jana, Mfuko huo umeweza kulipa hospitali zaidi ya bilioni 91 kwa kutoa huduma. Gharama hizo  zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Aidha ametoa wito kwa watanzania kubadilisha mfumo wa maisha kufuatia kuongezeka kwa wingi kwa wagonjwa wanaosumbuliwa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari ambayo yamekuwa yakiongeza gharama kubwa za matibabu kwa Mfuko huo.

Akizungumzia kuhusu waandishi wa habari kuungwa kwenye Mfuko huo Mkurugenzi huduma za Wanachama Hipoliti Lello amesema awali Mfuko huo ulitoa kifurushi maalum kwa wanahabari lakini walishindwa kutimiza vigezo na kutoa nafasi nyingine kwa umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), kukaa meza moja na Mfuko huo kuweka mikakati mipya ya namna wanahabari nchini wanaweza kufaidika na mpango wa serikali wa kupata bima ya afya kwa wote.

Amesema malengo ya baadae ya Mfuko huo ni kuongeza idadi kubwa ya wanachama kupitia sheria mpya ya bima  ya afya kwa wote ambapo ofisi yake imeanza mazungumzo na taasisi mbalimbali ili kuweza kuwaunganishaj watanzania kupitia makundi mbalimbali ikiwemo wakulima, wafugaji, wachimbaji madini wadogo wadogo .

Na WAF, DODOMA

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kurejeshwa kwa Toto Afya Kadi kutaleta matumaini mapya na uelekeo thabiti wa Bima ya Afya hususan kwa kundi la watoto ambalo linahitaji uangalizi wa pekee.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo tarehe 17, Desemba 2024 Jijini Dodoma, wakati akizindua vifurushi vitatu vya vya Bima ya Afya kikiwepo cha Toto Afya Kadi.

Waziri Mhagama amesema Mpango huo wa Toto Afya Kadi utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto za kiafya.

Waziri Mhagama ameongeza kuwa mpango wa sasa wa usajili wa Toto Afya Kadi utafanyika pia kwa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea mtoto husika hayupo shule, hii ni hatua kubwa na yakujivunia katika sekta nzima ya afya.

"Kila tunapokutana kwa ajenda ya ya Afya, tujue tunazungumzia usalama wa Taifa, maendeleo endelevu na uchumi wa nchi," amesema Mhe. Mhagama.

Mbali na kifurushi cha Toto Afya Kadi kilichozinduliwa leo, vifurushi vingine ni Ngorongoro chenye huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga kuhudumia watanzania.

Waziri Mhagama amesema mara baada ya uzinduzi wa vifurushi hivyo ajenda iliyopo mbele ni ubora wa huduma, huku akiwataka watoa huduma kuibeba ajenda hiyo na kutoa huduma zenye tija kwa maslahi ya umma wa watanzania ili waone umuhimu wa Bima na ifikapo 2030 Tanzania iwe imetimiza malengo ya kidunia.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa Vifaa Tiba na Dawa ambapo kwa sasa upatikanaji wa dawa ni wastani wa asilimia 86 ambayo imewezesha wananchi kunufaika na huduma hizo.

"Takriban vituo 9,826 nchi nzima, kati ya vituo hivyo, vituo 7,366 (sawa na 75%) ni vya Serikali, vituo 1,375 (sawa na 14%) vinamilikiwa na watu binafsi, vituo 1,006 (sawa na10.2%) vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na vituo 79 (sawa na 0.8%) vinamilikiwa na mashirika ya Umma. Vilevile kuna jumla ya kliniki 987 na Maabara 1,590", amefafanua Mhe. Mhagama.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu ameishukuru Serikali kwa kutekeleza maagizo ya Bunge huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kulisemea suala la Bima ya Afya.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka amesema kuzinduliwa kwa mfumo wa kidijitali kumewawezesha kushughulikia folio 1200 kwa dakika 45 tofauti na awali ambapo walishighulikia folio 800 tu kwa siku.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini Bw. Edga Gabriel amesema kuzinduliwa kutasaidia kutambua viashiria vya awali vya udanganyifu, hivyo wanaipongeza NHIF kwa ubunifu huo.

Serikali kupitia NHIF imefanikiwa kutengeneza mifumo ya kidijitali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.45 kwa kutumia wataalam wa ndani na kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 endapo wangetumia wataalam kutoka nje ya nchi.









 


Na : Jusline Marco : Arusha

Wataalamu wabobezi katika sekta ya Afya wametakiwa wametakiwa kutumia mikakati na mipango waliyoiweka katika kutekeleza sheria ya bima ya afya na kuwa na vyanzo endelevu vya kugharamia huduma za afya Nchini.

Mkurugenzi Idara ya Rasilimali watu kutoka Wizara ya Afya Issa Ng'imba ametoa rai hiyo wakati akifunga Kongamano la 7 la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kimataifa la Ugharamiaji Wa huduma za afya lililofanyika jijini Arusha ambapo amesema kwa umoja wao wanapasea kutekeleza kwa vitendo maadhimio hayo.

Aidha amesema maadhimio ni pamoja na kutumia utaalamu walionao Katika kuongeza rasilimali Fedha kwaajili ya kugharamia utekelezaji wa bima ya afya jwa wote,kuaandaa mkakati Wa utekelezaji wa UHI Ambao utabainisha majukumu na wajibu wa wadau wote wa sekta ya afya,kuhakikisha viwango Vya uchangiaji Wa wanachama Vinazingatia uwezo na kuwa na namna bora ya uchangiaji hususani katika sekta ziso rasmi.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa maadhimio hayo pia yamepitisha kuandaa mpango mkakati Wa kutekeleza dhana ya ulazima kwa watu wote kujiunga na bima ya afya ,kuandaa mpango shirikishi wa utoaji wa elimu kwa umma Kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya Kwa kuwashirikisha wadau wote.

"Tumekubaliana kuimarisha matumizi ya mifumo ya Tehama ili kuwezesha utekelezaji wa UHI hususani usajili wa wanachama Na vituo na uwasilishaji ,uchakataji na ulipajj wa madai sambamba kuwashirikisha wadau mbalimbalj katika dhana nzima ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote na utekelezajj huo hatumuachi mtu nyuma."Alieleza Mkurugenzi Idara ya Rasilimali watu kutoka Wizara ya Afya Issa Ng'imba


Meneja wa Mfuko  wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF ) Mkoa wa Kinondoni , Innocent Mauki (kushoto) akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea Banda la Mfuko huo namna ya kujaza fomu leo katika  maonesho ya  45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa mkoa wa  Dar es Salaam. 

Maafisa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) wakiwa wanendelea na kazi ya kusajili wananchi wanaojitokeza kupata huduma ya bima ya Afya katika  maonesho ya  45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa mkoa wa  Dar es Salaam. 
Wananchi wakiendelea kupata huduma ya Bima ya Afya katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)  leo katika  maonesho ya  45 ya Biashara ya Kimataifa  ya Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere  Barabara ya Kilwa mkoa wa  Dar es Salaam.