Articles by "MADAWA"
Showing posts with label MADAWA. Show all posts

 


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo ameshiriki katika sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mkoani Kilimanjaro.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge mwaka 2024 alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye amewaasa watumiaji wa bangi kuacha mara moja kwa ustawi wa maisha yao na taifa kwa ujumla.

Pia, amewaonya wakulima wa bangi nchini kuachana na Kilimo hicho na watakao kaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Sambamba na hilo, Mhe.Majaliwa amewaomba viongozi wa dini, Taasisi za Umma na binafsi, wazazi na walezi kushiriki  katika malezi ya vijana na kutoa elimu juu ya madhara ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii.




Na John Walter-Manyara

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) imetoa wataalamu sita wa saikolojia na masuala ya Ustawi wa jamii ambao wataungana na wataalamu wengine ambao wanaendelea kutoa huduma katika kambi tatu za waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe Hanang mkoani Manyara.

Akipokea wataalam hao, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, alisema kutokana na maafa yaliyowapata waathirika hao wa maporomoko na kupoteza ndugu na mali zao na  kupata msongo wa mawazo na hivyo kuhitaji kuwajenga kisaikolojia na kuwapa matumanini namna ya kuendelea na kurejea katika hali yao ya awali.

Pamoja na hilo Katibu Mkuu huyo amempongeza Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo kwa hatua hiyo na kusema kuwa timu hiyo itaungana na wataalam wengine waliopo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia wananchi hao kwa kuwapa huduma ya unasihi (ushauri) pamoja na elimu ya kujikinga na magonjwa ya afya ya akili wanapoendelea kuhudumiwa na Serikali.

“DCEA imetoa Wasaikolojia hawa ambao watajikita kutoa elimu kwa waathirika wa maafa yaliyotokea, hii ni hatua nzuri kwa kuwafikia na kuwashauri pale inapobidi ili kusaidia kutopata msongo wa mawazo na kupambana na changamoto ya afya ya akili,” alisema Dkt. Yonazi

Afisa Mwandamizi kutoka mamlaka hiyo, Daniel Kasokola, alisema Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo amechukua hatua ya kutuma timu hiyo kama sehemu ya kutekeleza wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka watanzania wote kuungana kuwataidia waathirika hao na anaamini kuwa,  timu hii  kwa kushirikiana na wataalam wengine itasaidia waathirika wa maafa hayo ili warejee katika hali zao za kawaida.

Naye mwanasaikolojia Deogtarias Ramale kutoa DCEA alisema huduma watakazozitoa zitawasaidia kuweza kukubaliana na kilichotokea na mazingira  ya sasa kutokana na kupoteza ndugu zao, mali na hatimaye  kurejea katika shughuli zao za kila siku.