Na Farida Mangube Morogoro 

Jumla ya wananchi 4,563 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kupitia Kambi Maalum ya Afya iliyofanyika katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, mkoani Morogoro.

Kambi hiyo iliyoanza Novemba 10 na kufungwa rasmi leo, Novemba 20, 2026, ilifanyika katika tarafa za Ngerengere, Mikese na Mkuyuni kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa za afya karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Mheshimiwa Hamiss Taletale, kwa juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa karibu na maeneo wanayoishi.

Aidha, Waziri Mchengerwa aliwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha hospitali zote nchini zinakuwa na upatikanaji wa dawa kwa kiwango cha asilimia 90 hadi 98 ili kuwawezesha wananchi kupata dawa wanazohitaji kwa uhakika.

Pia, alimtaka Mbunge Taletale kuendelea na juhudi za kuwasaidia wananchi wake kwa kujitolea kusogeza huduma za afya karibu nao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kambi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tatizo Waane, alisema kambi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuthibitisha umuhimu wa kuwafikishia wananchi huduma za uchunguzi na matibabu mapema.

Alisema kati ya wananchi 4,563 waliofanyiwa uchunguzi, watoto 533 walichunguzwa magonjwa ya moyo. Aidha, katika uchunguzi wa shinikizo la damu, watu 3,148, sawa na asilimia 69 ya waliopimwa, walibainika kuwa na kiwango cha juu cha shinikizo la damu.

Dkt. Waane alisema takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa changamoto ya shinikizo la damu katika jamii na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya afya, uchunguzi wa mara kwa mara pamoja na matibabu kwa watu wenye changamoto hiyo.

Katika huduma nyingine, wananchi 536 walifanyiwa kipimo cha Echocardiography (ECHO) kwa ajili ya kuangalia muundo na utendaji kazi wa moyo, huku watu 651 wakifanyiwa kipimo cha Electrocardiography (ECG) kwa ajili ya kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo. Vilevile, wananchi 483 walipata huduma za uchunguzi wa afya ya meno.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Hamiss Taletale, alisema wagonjwa 61 walipewa rufaa kwenda hospitali za mkoa, huku wagonjwa wengine 30 wakipewa rufaa kwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya matibabu zaidi.

Taletale, maarufu kama Babu Tale, alisema hadi sasa ametumia zaidi ya shilingi milioni 100 kugharamia matibabu ya wagonjwa waliopewa rufaa kwenda kwenye vituo vingine vya afya, fedha ambazo ni tofauti na gharama za kuendesha kambi hiyo.

Alisisitiza kuwa ataendelea kuwahudumia na kuwasaidia wananchi wa jimbo lake bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa wala kikabila.

Hata hivyo, alimuomba Waziri Mchengerwa kusaidia kutoa msukumo katika ujenzi wa barabara ya Bigwa–Kisaki ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, akieleza kuwa itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.



Share To:

Post A Comment: