Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal Juma (Shetta), ametangaza mkakati wa jiji wa kuimarisha usimamizi wa taka kwa kutumia mfumo wa uchumi wa mzunguko (Circular Economy), unaolenga kupunguza uchafuzi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuzigeuza taka kuwa rasilimali za kiuchumi.Akizungumza katika Mkutano wa Mameya wa Mtandao wa C40 Cities uliofanyika Antalya, Türkiye, Meya amesema jiji linaelekea kuachana na mfumo wa kawaida wa kukusanya na kutupa taka, badala yake kuimarisha utenganishaji, urejelezaji na uchakataji wa taka ili zitumike tena katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema upotevu wa chakula ni miongoni mwa changamoto zinazochangia mabadiliko ya tabianchi na kuathiri usalama wa chakula, huku akibainisha kuwa miji ina nafasi kubwa ya kutatua changamoto hiyo kupitia usimamizi wa masoko, mifumo ya taka na ushirikishwaji wa wananchi.
“Chakula kinapaswa kuwalisha watu, si kujaza madampo. Miji ina nafasi kubwa ya kukabiliana na upotevu wa chakula kwa sababu changamoto na suluhisho lake vinakutana mijini,” amesema.

Meya amefafanua kuwa takribani asilimia 25 ya uzalishaji wa gesi chafuzi jijini Dar es Salaam unatokana na shughuli zinazohusiana na taka, ikiwemo maji taka na utupaji wa taka ngumu. Aidha, amesema takribani asilimia 60 ya taka zinazozalishwa jijini hazikusanywi, huku asilimia 40 zikipelekwa katika eneo la utupaji taka la Pugu Kinyamwezi.
Kutokana na hali hiyo, Jiji limeweka mikakati ya kuhakikisha angalau asilimia 25 ya kaya zinatenganisha taka ifikapo mwaka 2030 na kuongeza kiwango cha urejelezaji kwa asilimia 50.
Pia, Jiji linaandaa uwekezaji katika miundombinu ya kuchakata hadi asilimia 50 ya taka za asili zinazozalishwa kila siku na kaya, hatua inayolenga kupunguza gesi ya Methane, kuzalisha mboji kwa ajili ya kilimo na kuongeza maeneo ya kijani.

Katika mkakati huo, Meya amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wajasiriamali wadogo, vikundi vya kijamii na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wanaojihusisha na ukusanyaji na urejelezaji wa taka, akieleza kuwa ushiriki wao utasaidia kufungua fursa mpya za ajira na kukuza uchumi.
Aidha, ameitambua C40 Cities kwa mchango wake katika kuimarisha programu za mazingira na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira, huku akihimiza miji kutumia takwimu katika kupanga mikakati na kujenga ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za mazingira.
“Tunapounganisha nguvu zetu kama miji, tunaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuboresha usalama wa chakula, kutengeneza maelfu ya ajira za kijani na kujenga mazingira safi na yenye afya,” amesema.
Amesisitiza kuwa kufikia dira ya Dar es Salaam kuwa Jiji lisilo na taka (Zero Waste City) kunahitaji uwekezaji katika teknolojia na miundombinu ya kisasa, ushirikiano wa wadau na ushiriki wa wananchi ili kujenga jiji safi, salama na endelevu.


Post A Comment: