Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yaliyohitimishwa kupitia mbio za NHIF Marathon 2026 zilizofanyika leo Novemba 29,2o26 katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.....
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema afya bora ya wananchi ni msingi wa kujenga taifa imara na kufikia malengo ya maendeleo, akisisitiza dhamira ya Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila vikwazo vya kiuchumi.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yaliyohitimishwa kupitia NHIF Marathon 2026 zilizoshirikisha takribani wananchi 10,000 jijini Dodoma, Mchengerwa ameipongeza NHIF kwa kutumia tukio hilo kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kujali afya zao.
Amesema safari ya miaka 25 ya NHIF imekuwa na mafanikio makubwa hususan ya utoaji na uboreshaji wa huduma za matibabu.
*Imekuwa ni safari ya kujenga taasisi yenye jukumu muhimu la kulinda afya za Watanzania na hii ndio dhamira inayoendana na misingi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ya kupambana na ujinga, maradhi na umaskin,”alisema.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, hususan kwa wananchi wasio na uwezo, ambapo takribani Shilingi bilioni 98 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia huduma za matibabu kwa makundi hayo.
Aidha, amesema kupitia kifurushi cha Bima ya Afya kwa Wote cha Shilingi 150,000 kwa kaya, Serikali inalenga kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wakulima, wafanyakazi, waendesha bodaboda, mama lishe na wafugaji, ili waweze kupata huduma za afya katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa amewahimiza wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kupima afya zao ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, akieleza kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya NHIF, hivyo umuhimu wa kuwekeza katika kinga.
Amewataka viongozi wa mikoa na wilaya pamoja na wadau wa afya kushirikiana kuhamasisha jamii kujali afya, akisisitiza kuwa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, afya bora ni jukumu la kila mdau na msingi wa ustawi wa taifa.


Post A Comment: