Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Taifa kimeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hatua inayotajwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CWT Taifa, Mwalimu Shaban Ambindwile,akiwa kwenye ziara katika Halmashauri hiyo ambapo amempongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kuwa na maono na dhamira ya dhati ya kuboresha elimu, akisema mikakati iliyowekwa inaonesha utayari wa Halmashauri hiyo katika kutatua changamoto zinazowakabili walimu.

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu, mipango iliyowasilishwa na Manispaa ya Kibaha ni ishara ya dhamira ya kuboresha mazingira ya walimu na wanafunzi, hatua aliyoitaja kuwa ushindi kwa Chama cha Walimu Tanzania.

Ameeleza kuwa Manispaa ya Kibaha imekuwa mfano katika kushughulikia changamoto za walimu na ni miongoni mwa halmashauri zinazochukua hatua kuhakikisha kero za walimu zinatatuliwa.

Akizungumza baada ya kupokea pongezi hizo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amesema halmashauri hiyo imeanzisha programu ya kujenga majengo ya utawala katika shule zote za msingi na sekondari ili kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu.

Dkt. Mawazo amesema Serikali Kuu na Halmashauri zinaendelea kutekeleza majukumu yake katika kuboresha sekta ya elimu, huku akisisitiza kuwa wazazi nao wanapaswa kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

Ameeleza kuwa Manispaa ya Kibaha ina jumla ya shule 58 za msingi na 24 za sekondari, ambapo shule 14 zimejengwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwaamba katika Mwaka wa fedha wa 2026/2027,Halmashauri imetenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: