Na. OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameongoza harambee ya ujenzi wa Uchira Boys Islamic Secondary School kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, iliyowezesha kupatikana Shilingi Milioni 655,347,500 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika Kata ya Kirua Vunjo Kusini, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Harambee hiyo ililenga kukusanya Shilingi Bilioni 1.2 katika awamu ya kwanza ili kuwezesha ujenzi wa madarasa, mabweni na miundombinu mingine ya msingi.
Kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 245,307,500 zilikuwa fedha taslimu na Shilingi Milioni 410,040,000 zikiwa ni ahadi.
Akiongoza harambee hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Novemba 25, 2026, katika ukumbi wa The SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amewataka Watanzania, taasisi, kampuni na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana katika uwekezaji kwenye sekta ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wa jamii katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwekeza katika elimu.
“Ujenzi wa shule hii unakuja wakati muhimu ambapo Serikali inajiandaa na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza kwa mwaka 2028, atia mabadiliko ya mfumo wa elimu ya msingi kutoka miaka saba kwenda miaka sita, hivyo kuongeza miundombinu ya shule ni hatua muhimu katika kukabiliana na mahitaji hayo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha miundombinu ya elimu, kuongeza nafasi za wanafunzi, upatikanaji wa walimu na vifaa vya kujifunzia. Amebainisha kuwa juhudi za wananchi wa Uchira na Registered Trustees of Masjid Salahudin za kujenga shule hiyo zinaunga mkono kwa vitendo mkakati wa Serikali wa kuimarisha huduma za elimu.
Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu kupitia shule za Uchira Islamic na juhudi zake za kuhamasisha maridhiano na amani nchini, huku akitoa wito kwa wadau wote kuunga mkono mradi huo kwa ajili ya maendeleo ya elimu na taifa kwa ujumla.










Post A Comment: