📌Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar yatembelea TBS.
Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imetembelea Shirika la Viwango Tanzania (TBS), katika ofisi zake zilizopo Ubungo, Dar-es-salaam, kwa lengo la kujifunza kuhusu shughuli za Shirika hilo na mifumo ya usimamizi wa viwango, hususan kanuni zinazohusu huduma za Metrolojia.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Hudhaima Mbaraka Tariq, ameongoza wajumbe katika ziara hiyo iliyowapa fursa ya kupata maelezo kuhusu shughuli za TBS na kanuni za metrolojia kutoka kwa wataalamu wa shirika hilo, pamoja na kushiriki majadiliano kuhusu utekelezaji wa majukumu hayo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, amesema Serikali inathamini ziara hiyo na kuamini kuwa uzoefu watakaobadilishana kati ya TBS na ZBS utasaidia kuimarisha mifumo ya viwango kwa manufaa ya Serikali zote mbili na wananchi kwa ujumla.
Manongi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya viwango ili kulinda afya za wananchi, kuongeza ubora wa bidhaa na kukuza ushindani katika soko, hatua itakayochangia maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Ashura Katunzi, ameeleza kuwa ushirikiano, uelewa, uwajibikaji na uwazi ni mambo muhimu katika kutekeleza majukumu ya taasisi za viwango na kukuza maendeleo ya uchumi wa Tanzania pamoja na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
“TBS itaendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mfumo wa vipimo unaoaminika, unaoweza kulinganishwa kimataifa na unaochangia katika maendeleo ya viwanda, biashara, sayansi na uchumi wa nchi.” AmesemaDkt Katunzi.
Aidha, wajumbe wa Kamati wametembelea maabara za TBS ili kujionea shughuli zinazofanyika katika eneo la vipimo na huduma za metrolojia. Ziara hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za viwango na kuimarisha ushirikiano kati ya TBS na ZBS katika kulinda afya za wananchi na kusaidia maendeleo ya viwanda na biashara.

Post A Comment: