Na Denis Chambi Tanga.

WAKATI Mkoa wa Tanga ukitajwa kuendelea kufunguka kiuchumi ukiwavutia wawekezaji  kutoka ndani na nje ya nchi Serikali imewataka wawekezaji hao kutoa kipaumbele kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya fani mbalimbali kutoka vyuo vya ufundi stadi (VETA) hatua ambayo itaongeza na kutanua soko la ajira kwa vijana.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Tanga Khalid Abdallah wakati akizungumza kwenye Mahafali ya wahitimu wa fani mbalimbali waliofadhiliwa na Shirika la maendeleo la Enabel katika Chuo cha ufundi stadi (VETA) kilichopo jijini Tanga ambapo amesisitiza fani mbalimbali zitahitaji wataalamu hivyo kipaumbele cha kwanza wapewe vijana wenye ujuzi.

"Tanga sasa hivi inafunguka kiuchumi na viwanda vingi vinarudishwa vyote hivyo vinahitaji wataalamu na tumeelekeza na kukubaliana kwamba nafasi nyingi  zitakazopatikana katika maeneo hayo  zipewe kwa vijana wa Tanga waliotoka VETA waingie viwandani wakafanye kazi" amesema

"Tanzania sasa inahitaji vijana ambao watajiajiri na kuajiriwa ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo yetu" ameongeza 

Aidha Abdallah amelipongeza Shirika hilo la Enabel kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa fursa mbalimbali za ajira kupunguza wimbi la vijana tegemezi katika jamii ambapo kupitia ujuzi wa fani mbalimbali  waliopata wataweza kujiajiri na kujipatia kipato.

Jumla ya Vijana 172 waliokuwa wakisoma kozi mbalimbali za muda mfupi katika Chuo cha ufundi stadi (VETA) jijini Tanga kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo la  Enabel kutoka nchini Ubelgiji  kwa awamu ya kwanza wamehitimu mafunzo hayo tayari kuingia katika soko la ajira.

Akizungumza katika mahafali hayo Mtaalamu Mshauri kutoka Shirika la  Enabel Thomas Aikaruwa amesema kuwa wameingia  mikataba na baadhi ya viwanda vilivyopo jijini Tanga kwa lengo la kuwachukua vijana watakaoweza kufanya vizuri baada ya masomo yao kwa lengo la kuwaajiri moja kwa moja hii ikiwa ni njia moja wapo ya kuwasaidia kuondokana na utegemezi katika familia pale wanapohitimu mafunzo yao kutoka vyuoni.


"Tuna furaha kuona kwamba kazi tuliyoianzisha kwa kushirikiana na wenzetu wa VETA tumeikamilisha, kuna baadhi ya viwanda na wadau ambao tumeingia nao miktaba na makubaliano maalum kwaajili ya kuwachukua vijana hawa lakini pia kuna kundi lingine litaenda SIDO kwaajili ya kuongezewa maarifa na ujuzi zaidi, na wengine walipoenda kufanya field baada ya kumaliza wamepata ajira moja kwa moja hili kwetu ni jambo kubwa sana" amesema.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yaliyohusisaha vijana172 kwa awamu ya kwanza Shirika litarudi tena kwa awamu ya pili ambapo litalenga vijana wanaofanya shughuli mbalimbali katika jamii ambao walikosa mafunzo hayo hivyo litawarasmisha na kuweza kuwapatia veti ili waweze kitambulika na kuingia katika soko la ajira wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Shirika hilo la Enabel kutoka nchini Ubelgiji linafanya shughuli zake katika Mikoa ya Tanga, Pemba Mwanza na Kigoma.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Meneja wa Rasilimali watu na utawala wa Kanda hiyo Neema Mkony ameeleza kuwa  jumla ya vyuo 14 vinaendelea kutoa mafunzo mbalimbali  ya ufundi stadi katika Mikoa ya Tanga , Kilimanjaro na Arusha  ambapo wanatarajia ifikapo mwaka 2027 kuwa na vyuo 20.

"VETA Kanda ya Kaskazini inahudumia Mikoa ya mitatu ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa sasa Kanda yetu ina vyuo 14 vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi  na kwa mwaka kesho 2027 kuanzia January tunatarajia kuwa na vyuo vipatavyo 23  ambavyo vitakamilisha vyuo kwenye wilaya zilizopo katika Kanda tunayoisimamia" amesema Mkony.
 
Ameongeza kuwa miongoni mwa vyuo vya ufundi stadi vilivyopo hapa nchini  VETA Tanga ni chuo kikongwe  ambachoo kimetoa wahitimi wa fani mbalimbali ambao  wanaendelea kufanya kazi katika taasisi na viwanda mbalimbali hapa nchini.

Aidha Mkony ameishukuru na kuipongeza Shirika hilo kwani halikuishia kuwapa fursa vijana pekee Bali pia limewawezesha na walimu wa chuo hicho kwa kuwajengea uwezo wa ufundishaji katika fani mbalimbali

"VETA Tanga ni miongoni mwa vyuo vikongwe na ni chuo chetu sisi Cha mfano katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi sisi VETA Kanda ya Kaskazini vijana wetu wamenufaika kupitia mradi wa Enabel  walimu wetu wameweza kujengwa uwezo kwahiyo tumenufaika" ameongeza.


Baadhi ya wahitimu wa waliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Enabel katika Chuo cha ufundi stadi VETA kilichopo jijini Tanga. 

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: