Na Mwandishi Wetu - Simanjiro

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mhe. Kaleya Melita Mollel ameitaka Kamati za Usimamizi wa Maafa wa Halmashauri hiyo kutekeleza yale yaliyomo kwenye Mpango wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa wa Halmashauri ya Simanjiro ili kuimarisha usimamizi wa maafa katika Wilaya hiyo.

Mhe. Mollel ameyasema hayo leo Oktoba 16, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati akizindua Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Wilayani ukiwa na lengo la kutoa miongozo na taratibu za kujiandaa na kukabiliana na maafa katika halmashauri ya wilaya na hasa katika kipindi hiki cha mvua za msimu.

“Nitoe wito nendeni mkatekeleze yaliyomo kwenye mpango huu, mpango huu usibaki kwenye makaratasi kwani ni nyezo muhimu ya usimamizi wa maafa katika halmashauri yetu” amesisitiza Mhe. Mollel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Kanali Selestine Masalamado amesema kuwa, mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya vihatarishi na uwezo wa wilaya wa kukabiliana na maafa, pamoja na historia ya matukio ya maafa yaliyoikumba Wilaya ya Simanjiro.

“Mpango huu ni matokeo ya mchakato shirikishi uliohusisha taasisi na wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa katika ngazi ya wilaya hivyo tunatarajia mpango huu utawezesha masuala mbalimbali ikiwemo uratibu wa shughuli za usimamizi wa maafa katika hatua zote za usimamizi wa maafa (Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali)” amefafanua Kanali Masalamado.

Aidha, ameongeza kuwa, maandalizi ya mpango huo ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 (Toleo la Mwaka 2025) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022, kwa kuweka mikakati madhubuti ya kujiandaa na kukabiliana na maafa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Idara ya Usimamizi wa Maafa, itaendelea kushirikiana nanyi, Wilaya ya Simanjiro katika shughuli za usimamizi wa maafa kwani usimamizi madhubuti wa maafa ni jukumu letu sote, kila mmoja ashiriki sasa na achukue hatua katika eneo lake, ili kulinda maisha na mali” ameongeza Kanali Masalamado.

Tathmini ya vihatarishi, uwezekano wa kutokea na uwezo wa kukabili maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro inaonesha kuwa, halmashauri hiyo inakabiliwa na majanga ya ukame, mafuriko, Migongano kati ya Wanyamapori na binadamu, moto magonjwa ya milipuko (binadamu, mifugo na wanyamapori) upepo mkali pamoja na mimea vamizi.


Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: