π Aagiza kila mkoa kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji
π Asisitiza mafanikio yapimwe kwa matokeo; si nyaraka
π Apongeza jitihada za Rais Samia katika kusukuma mbele ajenda hiyo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuifanya ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia kuwa miongoni mwa vipaumbele vya mikoa yao, kwa kuweka mikakati mahsusi itakayoongeza kasi ya matumizi ya nishati hiyo miongoni mwa wananchi.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 28, 2026, jijini Dodoma, wakati wa Kikao Kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara kujadili ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini.
"Mafanikio ya mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia hayatapimwa kwa uwepo wa nyaraka, bali kwa matokeo halisi yanayoendana na Dira ya Taifa na mipango ya maendeleo ya nchi hivyo tuhakikishe kuwa wananchi katika maeneo yetu wanatumia nishati hii ambayo ni muhimu kwa afya na mazingira yetu." Amesema Mhe. Dkt.Nchemba
Amesema hatua na mageuzi yaliyofikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia yanatokana na jitihada za Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa ajenda hiyo na kuipa msukumo mkubwa kitaifa na kimataifa, hatua iliyoliletea Taifa heshima miongoni mwa mataifa mengine.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuupa kipaumbele mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa maslahi mapana ya Taifa, hususan katika kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuboresha ustawi wa jamii.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kuongeza uelewa na matumizi ya nishati hiyo, bado kuna kazi kubwa ya kufanya, hususan katika mikoa ambayo matumizi yake bado yako chini, ikiwemo Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora na Katavi.
Akizungumzia matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi, amesema kati ya taasisi 31,000, ni taasisi 2,700 pekee zinazotumia nishati hiyo, zikiwemo shule na vyuo, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuweka malengo mahsusi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda hiyo.
Aidha, amezitaka Wizara zinazohusika na mkakati wa nishati safi na Wakuu wa Mikoa kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mei 8, 2024, kwa kutathmini hatua zilizofikiwa na kuweka mikakati ya kuongeza matumizi.
Amesisitiza kuwa Wakuu wa Mikoa ni kiungo muhimu kati ya Serikali Kuu na wananchi, hivyo kila mkoa unapaswa kuandaa mpango mahsusi unaozingatia mazingira na mahitaji ya eneo husika, ukiambatana na viashiria vinavyopimika ili kufuatilia maendeleo ya utekelezaji.
Vilevile, amewataka viongozi kuendeleza elimu na uhamasishaji bila kupuuza mila na mazoea ya wananchi katika matumizi ya nishati ya kupikia, ili kuwawezesha kuelewa umuhimu wa mabadiliko na kuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Waziri Mkuu amepongeza Wizara ya Nishati kwa jitihada zinazofanyika katika kusukuma mbele ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi.


Post A Comment: