Na: OWM–TAMISEMI, Tunduma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za maingilio na mchepuko mkoani Songwe, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri pamoja na usafirishaji wa bidhaa. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 6 zitatumika Wilaya ya Momba, ambapo bilioni 3 zitatumika Tunduma na bilioni 3 kwa maeneo mengine ya wilaya hiyo, huku bilioni 9 zikielekezwa katika wilaya za Mbozi, Ileje na Songwe.
Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 15, 2026, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM–TAMISEMI katika kutatua kero zilizowasilishwa na wananchi wa Tunduma wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Songwe.
Amefafanua kuwa ujenzi huo utasaidia kupunguza msongamano katika barabara ya Tunduma–Mpaka wa Zambia, barabara kuu ya TANZAM inayounganisha Igawa–Songwe–Tunduma, pamoja na barabara ya Mpemba–Tunduma, hususan eneo la mizani ya Mpemba.
“Mhe. Makamu wa Rais, TAMISEMI tuko tayari. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kujenga barabara za maingilio na mchepuko mkoani Songwe,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu na kupunguza changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi na wafanyabiashara, hasa katika maeneo yenye shughuli nyingi za biashara na usafirishaji wa mizigo ya ndani na kuvuka mipaka.
Katika sekta ya afya, Prof. Shemdoe amemueleza Makamu wa Rais kuwa OWM–TAMISEMI imetekeleza maelekezo ya kutenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ivuna, kilichopo katika Jimbo la Momba, ambalo Mbunge wake ni Mhe. Condester Sichalwe. Amesema uwekezaji huo utaboresha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Kuhusu elimu, Prof. Shemdoe amesema Serikali inakamilisha ujenzi wa shule ya saba ya ghorofa, huku shule sita zikiwa zimekamilika. Ujenzi huo umewezesha kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya nafasi wakati wa kupokea wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kwa mfumo wa double cohort, utakaowahusisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na darasa la sita kutokana na utekelezaji wa mtaala mpya. “Halmashauri ya Mji wa Tunduma iko tayari kuwapokea wanafunzi hao,” amesema.
Aidha, Prof. Shemdoe amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduma kwa ajili ya wodi ya mama na mtoto, ili kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma za afya ya uzazi. Tunduma, kama ilivyo Katoro, ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo, watoto 1,500 huzaliwa kila mwezi; 800 katika vituo vya Serikali na 700 katika vituo vingine.
Prof. Shemdoe amesema uwekezaji huo katika barabara, elimu na afya unaonesha dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za kijamii na miundombinu, kupunguza changamoto za wananchi na kuweka mazingira bora kwa shughuli za kiuchumi na kijamii mkoani Songwe.










Post A Comment: