Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, amewasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu inayolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Angola.
Rais Lourenço amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, ambako amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).
Oktoba 29, 2026, Rais Lourenço atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Dar es Salaam. Baada ya mapokezi hayo, viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi ya pande mbili kuhusu masuala yenye maslahi kwa nchi zao, kabla ya kukutana na waandishi wa habari kueleza makubaliano na matokeo ya mazungumzo yao.
Aidha, Oktoba 30, 2026, Rais Lourenço ataelekea Dodoma, makao makuu ya nchi, ambako atashiriki pamoja na mwenyeji wake katika hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba.
Ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano kati ya Tanzania na Angola katika maeneo yenye manufaa kwa mataifa hayo mawili.


















Post A Comment: