DAR ES SALAAM. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amewapongeza waandaaji wa tuzo za Supply Chain, Mobility & Logistics Awards (SML Awards 2026) kwa kuanzisha jukwaa linalowaunganisha wadau muhimu wa uchumi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho la matatizo yanayoikabili sekta ya ugavi, usafirishaji na uchukuzi.

Othman alitoa pongezi hizo wakati akihutubia hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam, akisema waandaaji wamefanya jambo la kipekee kwa kuifanya hafla hiyo kuwa zaidi ya tukio la kukabidhi tuzo kwa washindi.

Alisema jukwaa hilo limewapa wadau nafasi ya kukutana, kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na uchumi, pamoja na kuchambua vikwazo vinavyoikabili sekta ya ugavi, usafirishaji na masoko, hatua inayoweza kusaidia kutafuta ufumbuzi na kukuza shughuli za biashara nchini.

Aidha, aliipongeza bodi ya SML Awards pamoja na washindi wote waliotambuliwa katika hafla hiyo, akiwahimiza kuendeleza juhudi zao ili kuhakikisha jukwaa hilo linakua na kufikia viwango vya juu zaidi katika kutambua mchango wa wadau na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SML, Amon John Mtonyi, alisema lengo kuu la tuzo hizo ni kutambua na kuthamini mchango wa wadau wanaojihusisha na shughuli za ugavi, usafirishaji na uchukuzi katika nafasi mbalimbali.

Mtonyi alisema jumla ya kampuni 54 zimetambuliwa kwa mchango na mafanikio yao kupitia tuzo hizo, akieleza kuwa mpango huo pia unalenga kujenga jukwaa la biashara litakalowaunganisha wadau muhimu wa uchumi na kukuza ushirikiano pamoja na uwekezaji katika sekta husika.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: