Na Mwandishi Wetu, TANGA



MAAFISA Elimu Kata katika Jiji la Tanga wameanza kushirikishwa katika mafunzo ya walimu yanayotolewa kupitia mradi wa Tanga Yetu, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa mafunzo hayo na hatimaye kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na Taasisi ya Tanzania Centre for Education kupitia mradi wa Tanga Yetu, unaodhaminiwa na Botnar Foundation kwa kushirikiana na Inovet, ukiwa na lengo la kuchangia kuboresha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi pia yakilenga

Pia yakilenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia na rasilimali za kidijitali katika ufundishaji, huku Maafisa Elimu Kata wakipewa nafasi ya kufuatilia mafunzo hayo ili waweze kuyasimamia wanaporejea shuleni.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Centre for Education Yusuf Ogutu alisema ushiriki wa Maafisa Elimu Kata ni muhimu kwa kuwa wao ndio wanaohusika na usimamizi wa shughuli za elimu katika kata zao.



Alisema kupitia ushiriki huo, Maafisa Elimu Kata wataweza kufahamu maudhui yanayofundishwa, changamoto zinazowakabili walimu na hatua zinazoweza kuchukuliwa kuhakikisha mafunzo yanakuwa na matokeo yaliyokusudiwa.

“Ni jambo la muhimu kwa Maafisa Elimu Kata kujua kinachofanyika katika mafunzo haya ili wanaporudi shuleni waweze kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake,” alisema.

Kwa mujibu wa mtoa maelezo huyo, mafunzo hayo pia yanawalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia Digital Learning ili kurahisisha upatikanaji wa mitihani, notisi, vitabu na rasilimali mbalimbali za kujifunzia zinazopatikana kwenye mitandao.



Alisema matumizi ya teknolojia yatawasaidia walimu kupata nyenzo mbalimbali za kufundishia na kujifunzia kwa urahisi, pamoja na kuwawezesha kutumia mifumo ya E-Learning katika kuboresha ufundishaji.

Aidha, alisema Maafisa Elimu Kata watakuwa na jukumu la kufuatilia ushiriki wa walimu katika mafunzo hayo, kutambua walimu ambao hawajashiriki na kuhakikisha maudhui yaliyofundishwa yanafanyiwa kazi shuleni.

“Maafisa Elimu Kata ndio wanaosimamia shule katika kata zao. Kupitia wakuu wa shule wataweza kufuatilia ni walimu gani wamehudhuria mafunzo na ni kwa kiwango gani wanatumia maarifa waliyopata,” alisema.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mafunzo yanayotolewa hayabaki darasani pekee, bali yanafikia wanafunzi kupitia maboresho ya ufundishaji na matumizi sahihi ya rasilimali za kidijitali.



Kwa upande mwingine, Maafisa Elimu Kata walipata fursa ya kufuatilia changamoto zinazowakabili walimu wakati wa kutumia teknolojia na nyenzo mbalimbali za kidijitali, ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi ambapo mafunzo hayo yanaendelea kwa awamu kulingana na masomo yanayolengwa.



Jana ilikuwa siku ya mwisho ya mafunzo kwa walimu wa masomo ya Historia, Jiografia na Business Studies, huku wiki hii yakitarajiwa kuendelea kwa walimu wa masomo ya Sayansi, Fizikia, Baiolojia, Kemia na Hisabati.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: