Mkuu wa Wilaya ya Tarime, (DC) Meja Edward Gowele, akizungumza na wakazi wa vijiji vya Matongo na Nyangoto kuhusu mradi huo wa TSF.
Mkurugenzi wa Shirika la Sheria na Haki za Binadamu la Tuwakombowe Paralegal (TPO) linalofanya shughuli zake katika wilaya za Tarime na Rorya, Bonny Matto (aliyevaa kofia ya kaki), akizungumza na wananchi katika eneo la uthamini huo. Kulia mbele aliyevaa kofia nyeusi ni Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele.
Meneja Mahusiano ya Jamii wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, akizungumza katika mkutano wa kuelimisha wakazi wa Matongo na Nyangoto kuhusu mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kuhifadhi Mabaki ya Uchimbaji TSF.
Muonekano wa sehemu ya eneo linalofanyiwa uthamini kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa TSF.

**

#Wakazi zaidi ya 350 wafanyiwa uthamini kupisha ujenzi wa Bwawa la kuhifadhi taka sumu

Wananchi zaidi ya 350 wa vijiji vya Matongo na Nyangoto vilivyopo Kata ya Matongo Wilayani Tarime  Mkoani Mara wamefanyiwa uthamini kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Bwawa la Kuhifadhi Taka -Sumu (Tailings Storage Facility – TSF) jipya la Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

 Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 16,2026 wilayani Tarime, Mkuu wa Wilaya ya hiyo , Meja Edward Gowele (DC) amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa kwa ajili ya kazi ya kufanyiwa uthamini wa mali zao ili waweze kupisha ujenzi wa bwawa hilo na kufungua milango kwa ajili ya kulipwa fidia.

 “Mwitikio ni mkubwa na unaridhisha, hadi leo watu 350 wafamefanyiwa uthamini kazi hii ni kubwa kwa ajili ya watu watakaopisha ujenzi wa bwawa hili na shughuli hii inaendelea vizuri,”alisema Meja Edward Goweley.

 Alisema  uthamini unafanyika katika vijiji vya Matongo na Nyangoto vilivyopo Kata ya Matongo Wilayani, Tarime ili kuwezeshwa mgodi huo kuanza ujenzi wa bwawa hilo kwenye eneo hilo.

 Aliongeza kwamba kazi hiyo ilianza Agosti 24, mwaka huu na inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 60, ambapo eneo lenye ukubwa wa ekari 419 linahitajika ili kujenga mradi huo mkubwa wa kuhifadhi taka sumu.

 Aidha, alisema kwamba katika kuhakikisha haki, uwazi, usawa, sheria na uwajibikaji vinazingatiwa kwa pande zote zinazohusika, Barrick imewashirikisha watetezi wa haki za binadamu kutoka mashirika ya ndani kama waangalizi wa uthamini huo.

 “Uwazi ni mkubwa na hata kuna watu wa haki za binadamu na vyombo vingine vya serikali, ikiwemo TAKUKURU ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote,” alisisitiza Meja Gowele.

 Wakati uthamini huo unaanza Agosti 24, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele alitangaza katazo la serikali kwa wananchi kutofanya uendelezaji wowote katika eneo hilo ambalo lipo katika leseni ya mgodi huo wa Barrick North Mara.

 “Uzuri ni kwamba kazi hii ya uthamini imekuwa shirikishi kuanzia ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya,” alisema Meja Gowele.

 Alitoa onyo kwa wakazi wa Tarime na vitongoji vyake hasa vikundi vya watu maarufu kama Tegesha wanaofanya mchezo wa kuweka miradi , nyumba na mazao sehemu ambayo zimefanyiwa uthamini kuacha mchezo huo mara moja.

 Onyo hilo la Mkuu wa Wilaya wa Tarime , Meja Gowele lilikwenda mbali mpaka kwa taasisi za serikali ambazo zinaendeleza baadhi ya miradi au shughuli kama vile Tanesco kwa kupeleka umeme kwenye nyumba ambazo zipo tayari kwenye uthamini kuondoa mara moja.

 Aidha, aliwataka wataalamu na wasimamizi wa mradi huo kutenda haki na kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote unaofanyika hadi hatua ya malipo ya fidia.

 Pamoja na mambo Shughuli hiyo ya uthamini inatekelezwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 Kabla ya kuanza uthamini huo, Serikali ilishirikiana na Mgodi wa  Barrick North Mara kuendesha mikutano ya kuelewesha na kuhamasisha wananchi wa maeneo hayo kuhusu ujio wa mradi huo.
 
Mgodi wa  Barrick North Mara unaendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

 Mradi wa ujenzi wa TSF ni muhimu katika upanuzi na uendelevu wa shughuli za mgodi huo kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi. Kwa mujibu wa Barrick, utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba maisha ya Mgodi wa Dhahabu wa  Barrick North Mara yameongezeka kutoka mwaka 2030 hadi 2041. Unalenga kuendana na uendelevu wa mgodi huo baada ya tafiti za Barrick kurefusha maisha ya Mgodi wake.

 Mabwawa ya kuhifadhi Taka-Sumu (Tailings facilities), ambayo ni miundombinu mikubwa iliyosanifiwa kitaalamu kwa ajili ya kuhifadhi mabaki yanayotokana na uchakataji wa madini, ni miongoni mwa maeneo yenye hatari kubwa zaidi za kiusalama katika migodi.

 Barrick inatumia mfumo madhubuti wa viwango vya kimataifa wa usimamizi wa mabaki ya uchimbaji unaotanguliza usalama wa watu na mazingira hupewa kipaumbele katika kuchagua maeneo, usanifu, ufuatiliaji, uendeshaji na hatimaye kufungwa kwa miundombinu ya kuhifadhi mabaki ya uchimbaji.

 Kama ilivyo katika shughuli zake za uendelevu, Barrick imekuwa ikishirikiana kwa karibu na jamii zinazozunguka migodi yake ili kuhakikisha uwekezaji wao unaleta manufaa ya kudumu kwa jamii.

 Katika Mgodi wa Barrick North Mara nchini imewekeza takribani Dola za kimarekani 65  milioni kujenga mitambo miwili ya kisasa ya kutibu maji katika maeneo ya kuhifadhi mabaki ya uchimbaji.

 Kampuni ya Barrick imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka migodi yake na Taifa kwa ujumla, huku ikiongoza kwa ulipaji wa Gawio, mrahaba , kodi mablimbali na mapato yasiyotokana na kodi serikalini.

 Tangu Ubia wa Barrick na Twiga uanze mwaka 2019, Barrick imewekeza zaidi ya  Dola za Kimarekani bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania, kwa mujibu wa takwimu zilizopo.

 Kampuni ya Barrick pia imekuwa ikitekeleza Sera ya Ushurikishwaji Watanzania katika mnyororo wa sekta ya madini (Local Content) kwa vitendo, ambapo inafanya ununuzi wa bidhaa za uzalishaji kwa asilimia zaidi ya 90 kutoka kwa wazabuni wa ndani, huku asilimia 96 ya wafanyakazi wake wakiwa Watanzania, wakiwemo wanaotoka maeneo ilipo migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu.
Share To:

Post A Comment: