Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekutana na kufanya Mafunzo ya siku mbili yanayolenga kubadilishana uzoefu na kuimarisha uelewa kuhusu majukumu na utekelezaji wa Sheria katika sekta ya usafiri.
Mafunzo hayo yanafanyika tarehe 17 na 18 Septemba, 2026, ambapo Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamefanya ziara LATRA kwa lengo la kufahamu kwa kina shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka hiyo pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,Bw. Habibu Suluo, amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa LATRA inasimamia sekta za usafiri wa barabara, reli na usafiri wa waya, ambazo utekelezaji wake unategemea Sheria, kanuni na taratibu mbalimbali.
Aidha, uelewa wa pamoja kati ya LATRA na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali utasaidia kuboresha utekelezaji wa Sheria, utoaji na usimamizi wa leseni, utatuzi wa migogoro pamoja na namna Mamlaka inavyowasiliana na wananchi na wadau.
“Wakifahamu namna tunavyotekeleza majukumu yetu, maeneo tunayoyasimamia na changamoto tunazokutana nazo, itawasaidia kutushauri vizuri na kuhakikisha Serikali haijiingizi kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima,” amesema Bw. Suluo.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali wa Mkoa- Morogoro Bw. Iddi Mgeni, kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema Mafunzo hayo yanalenga kujifunza namna LATRA inavyotekeleza majukumu yake, mawanda ya kazi na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria.
“Kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sisi ni washauri wakuu wa Serikali katika masuala ya kisheria. Kwa hiyo, kufahamu LATRA inafanya nini na changamoto inazokutana nazo kutatusaidia katika kutoa ushauri unaoendana na mahitaji halisi ya Mamlaka,” amesema Bw. Mgeni.
Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuhusu Utekelezaji wa Sheria katika Usafiri yamefanyika kuanzia tarehe 17 hadi 18 Septemba, 2026 katika Ofisi za LATRA jijini Dar es Salaam, ambapo Washiriki wanatarajiwa kutembelea baadhi ya mifumo ya LATRA ili kujifunza namna inavyofanya kazi na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na ushauri wa kisheria.




























Post A Comment: