Na Oscar Assenga,TANGA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, ametaka elimu ya kupinga rushwa ianze kutolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi wakiwa na umri mdogo ili kuwajengea maadili ya uadilifu, uaminifu, uwajibikaji, uzalendo na kuipenda nchi yao.
Dk. Burian alitoa kauli hiyo Agosti 6, 2026, wakati wa fainali ya shindano la Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 mkoani Tanga, lililofanyika katika Shule ya Ufundi Tanga (Tanga Technical Secondary School).
Alisema kuwafundisha wanafunzi masuala ya rushwa kuanzia wakiwa darasa la tatu kutawajengea msingi imara wa kuchukia na kukemea vitendo vya rushwa, hivyo kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Alisema wanafunzi tayari wanaonesha uelewa mkubwa kuhusu madhara ya rushwa kwa maendeleo ya taifa.
“Kama mlivyowasikia wanafunzi wakijieleza, wameonesha namna rushwa inavyodumaza maendeleo. Inaweza kusababisha kujengwa kwa madaraja mabovu kwa sababu ya kumpa kazi mkandarasi asiye na sifa. Mwisho serikali hudhani imetekeleza maendeleo, kumbe ni maendeleo ya magumashi,” alisema.

Dk. Burian, ambaye aliwakilishwa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Tanga, Emanuel Kisongo, alisema walimu wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wanafunzi kwa kuwalea katika misingi ya maadili mema na kuwafundisha athari za rushwa kwa jamii na taifa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata, alisema shindano la Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 linalenga kujenga kizazi chenye uadilifu kupitia wanafunzi wa shule za msingi.
Alisema maadili yanayojengwa kwa watoto yatawasaidia kukua wakiwa raia wanaochukia rushwa na kuzingatia misingi ya haki na uwajibikaji.
“Tunataka kujenga kizazi kitakachokuwa sehemu ya suluhisho la tatizo la rushwa badala ya kuwa sehemu ya tatizo. Vitendo vina nguvu kubwa katika kujenga maadili kuliko maneno pekee,” alisema.
Ndwata alisema kuanzishwa kwa klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi kumeongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu masuala ya rushwa.
Alisema wakati wa mashindano hayo wanafunzi walikuwa wakisahihishana wenyewe kuhusu masuala yanayohusu rushwa, jambo alilosema ni ishara ya mafanikio ya programu hiyo na kwamba wako tayari kuwaelimisha wengine.
Aidha, aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza elimu dhidi ya rushwa, akisema familia ina nafasi kubwa katika kujenga maadili ya kizazi kijacho.
Mratibu wa mashindano hayo Frank Mapunda alisema Shule ya Msingi Kombezi iliibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia kombe kubwa pamoja na fedha taslimu Sh200,000.
Alisema mshindi wa pili alikuwa Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Msingi Bombo iliyopata kombe dogo na Sh150,000, huku Shule ya Msingi Chumbageni ikishika nafasi ya tatu na kujishindia ngao ya glasi pamoja na Sh100,000.
Nafasi ya nne ilichukuliwa na Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Msingi Nguvumali iliyopata ngao ya plastiki pamoja na Sh50,000.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkwakwani Faraja Mwagike alisema kuanzishwa kwa klabu za wapinga rushwa kumewaongezea wanafunzi uadilifu, ujasiri na kuwajengea msingi wa kuwa raia wema watakaoheshimu sheria na kutenda haki.
Naye mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisosora, Mariam Juma, alisema klabu hizo zimechangia kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na taifa.
“Ni muhimu wigo wa klabu hizi ukaongezwa ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na elimu hii na ujumbe uwafikie wote,” alisema.


Post A Comment: