Na Munir Shemweta
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania (IST), ambapo pande hizo zilijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya Upimaji Ardhi na sekta ya ardhi nchini.
Ujumbe wa IST ulioongozwa na Rais wa taasisi hiyo, Dkt. Julian Magezi Ijumulana na Upande wa Wizara ya Ardhi uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Upimaji Ardhi ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor, ulimtembelea Waziri Dkt. Akwilapo kwa lengo la kujitambulisha.
Aidha, ujumbe huo ulimuelezea Mhe Dkt Akwilapo mikakati ya taasisi hiyo, ikiwemo maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 45 ya kuanzishwa kwake pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka unaotarajiwa kufanyika Novemba 2026 katika Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza katika kikao hicho, Julai 2, 2026 jijini Dar es Salaam Dkt. Akwilapo alisema ameyapokea mawazo na mapendekezo yaliyowasilishwa na Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi kwa kuzingatia maslahi ya sekta ya ardhi na maendeleo ya nchi.
Aidha, Waziri Dkt. Akwilapo alisisitiza kuwa swala la sheria ya Upimaji ardhi sura 324 na usajili wa Wapima ardhi sura 270 amelipokea na atafanyia kazi kwa haraka kwani Wapima Ardhi wana nafasi muhimu katika kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi nchini kupitia upimaji sahihi.

Post A Comment: