Mlezi wa APSP na Kamishna Mstaafu wa Sera za Ununuzi wa Umma, Dkt. Fredrick Asumile Mwakimbinga,Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (APSP) umefanyika jijini Arusha ukiwa na lengo la kupokea taarifa za uongozi, kujadili utekelezaji wa maazimio, fedha na bajeti, pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ushiriki wa makundi maalum na biashara ndogo na za kati (SMEs) katika fursa za ununuzi wa umma.
Akifungua mkutano huo, Mlezi wa APSP na Kamishna Mstaafu wa Sera za Ununuzi wa Umma, Dkt. Fredrick Asumile Mwakimbinga, alisema zaidi ya asilimia 70 ya fedha za Serikali hupitia katika shughuli za ununuzi, hivyo aliwataka wataalamu wa sekta hiyo kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia maadili ya taaluma na kulinda heshima ya taasisi zao.
Dkt. Mwakimbinga pia aliwahimiza wanachama kuendelea kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi kwa kuzingatia sheria na matumizi ya teknolojia, kushiriki kutoa elimu kwa umma, kusimamia migogoro ya mikataba, kufanya ukaguzi wa bidhaa na kuzuia bidhaa bandia ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati.
Alisema kaulimbiu ya mkutano huo, inayohusu kuimarisha ushiriki wa kitaaluma na kuwezesha makundi maalum pamoja na SMEs kunufaika na fursa za ununuzi wa umma, inalenga kuwafanya wataalamu kuwa kiungo muhimu kati ya sheria, urasimishaji wa biashara na utekelezaji wa maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya APSP, Dkt. Emmanuel Urembo, alisema mustakabali wa taaluma hiyo unategemea uwezo wa wataalamu kuendana na maendeleo ya teknolojia, kuzingatia maadili na kutoa ushauri wa kimkakati. Alibainisha kuwa chama kina wanachama zaidi ya 2,200 na kimepata mafanikio ikiwemo kusaini mikataba ya ushirikiano, kulipa deni la kiwanja la shilingi milioni 134 na kusajili nembo ya chama kupitia BRELA.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria na Uzingatiaji kutoka BRELA, Wakili Lamecky Nyangi Samson, alisema wataalamu wa ununuzi wana mchango mkubwa katika kuhamasisha urasimishaji wa biashara kwa kuzingatia sheria na kuunganisha wafanyabiashara na fursa zinazotokana na ununuzi wa umma.
Akifunga mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Denis Kwame Simba, aliwataka washiriki kutumia mifumo ya kielektroniki kwa ufanisi, kuzingatia uwazi, ushindani na thamani ya fedha, kutenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum, kusimamia vihatarishi, kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kuzingatia masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.
Post A Comment: