HALMASHAURI za Wilaya, Miji na Jiji mkoani Tanga, zimeagizwa kuzuia vyanzo vinavyosababisha hoja zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Agizo hilo limetoa leo Juni 30, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt Batilda Burian, alipozungumza kwenye vikao maalum vya kujadili hoja za CAG katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri za Lushoto na Bumbuli.
Amesema, taarifa za CAG kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, inaonesha halmashauri hizo zimefanikiwa kupata hati inayoridhisha, ikiwa ni Ishara ya ufanisi, weledi na kujituma kwa watumishi na watendaji.
Amesema, hali hiyo inapaswa kuendelezwa ili kufikia malengo msingi ya Serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hata hivyo, Mhe. Balozi Dkt Batilda amesema, pamoja na mafanikio hayo, halmashauri hizo zinatakiwa kudhibiti vitendo vinavyosababisha hoja za ukaguzi.
Awali, taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Nje, Mkoa wa Tanga, Hamu Mwakasola, ilieleza kuwa kutolewa hati inayoridhisha haimaanishi kuwepo mifumo mizuri ya udhibiti wa ndani, bali kutokuwepo dosari kubwa wakati wa ukaguzi.
“Inamaanisha hapakuwa dosari kubwa zilizobainika wakati wa ukaguzi ambazo zingemzua Mkaguzi kutoa maoni, au kumlazimu kutoa hati yenye mashaka au hati mbaya,” amesema
Naye Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Tanga, Rashid Mchatta, pamoja na mambo mengine, amewahimiza watumishi na umma, kuendeleza mahusiano mema ili kuongeza ufanisi na tija mahali pa kazi.
Amesema, viongozi, watendaji na watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapaswa kutambua ‘uzito’ wa hadhi ya Ofisi ya CAG katika ukaguzi wa hesabu uliopo katika ngazi za kimataifa.
Mchatta amesema utambuzi wa ubora huo utachangia kuboresha utendaji kazi na kupunguza kwa kiasi kikubwa hoja za ukaguzi, hali itakayoifanya CAG kutekeleza vema wajibu wake wa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi husika.





.jpg)

Post A Comment: