📌 Waziri Ndejembi asema mradi utaimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme
📌 Mradi unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026
📌 MD TANESCO asema Shirika limevunja rekodi kwa kuunganisha wateja zaidi ya laki nane mwaka 2025/26
Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma wenye urefu wa kilometa 345 umefikia asilimia 89 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026, hatua itakayoongeza uwezo wa kusafirisha umeme na kuimarisha uthabiti wa Gridi ya Taifa.
Akikagua maendeleo ya Mradi huo Julai 1, 2026, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), amesema mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji wa kimkakati wa Serikali unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme nchini na kuongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kuhudumia mahitaji yanayoendelea kuongezeka.
Amesema njia hiyo ya kusafirisha umeme ina umuhimu mkubwa kutokana na kuwezesha usafirishaji wa umeme unaozalishwa na Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Aidha, Waziri Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya umeme ili kuhakikisha huduma ya umeme wa uhakika inaendelea kuwafikia Watanzania na kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za uzalishaji.
“Serikali imeona mahitaji ya umeme nchini yanazidi kuongezeka, hivyo ujenzi wa njia hii ya umeme ni muhimu sana kwani utaleta uthabiti katika Gridi ya Taifa,” amesema Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Razalo Twange, amesema ongezeko la uwekezaji katika miundombinu ya umeme limechangia kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaounganishiwa huduma, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26 Shirika limeandika historia kwa kuwaunganishia umeme zaidi ya wateja laki nane.
“Haijawahi kutokea tangu Tanzania ipate uhuru. Hii inaonesha mahitaji ya umeme yameongezeka, na hivyo sisi tunaendelea kuongeza miundombinu ya umeme,” amesisitiza Bw. Twange.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Mradi, Mha. Newton Mwakifamba, amesema kazi zinaendelea vizuri na zinatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026, kwa mujibu wa ratiba ya mkataba.










Post A Comment: