Rais wa Jamhuri ya Muungwana wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan (katikati)akikabidhiwa gawio la Sh.bilioni 15 kutoka kwa  Mwenyekiti wa Bodi ya Tiper Balozi Mathias Chikawe(kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Tiper  Mohamed Mohamed (kulia) wakati wa hafla ya Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam ambapo mashirika na taasisi mbalimbali ambazo Serikali inahisa wamekabidhi gawio serikalini.

****************

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER) imeonyesha ukuaji mkubwa wa biashara baada ya kuongeza gawio lake kutoka Shilingi milioni 500 mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 15 kwa Serikali mwaka 2025, hatua iliyoifanya kutoa gawio la rekodi la Shilingi bilioni 30 kwa wanahisa wake wawili.

Gawio hilo lilikabidhiwa Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya mashirika na taasisi ambazo Serikali ina hisa kuwasilisha gawio kwa Serikali. Kati ya kiasi hicho, Serikali na Oryx Energies, ambao kila mmoja anamiliki asilimia 50 ya TIPER, walipokea Shilingi bilioni 15 kila mmoja.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema TIPER imeandika historia kwa kutoa gawio kubwa zaidi kuwahi kutolewa tangu kampuni hiyo ianze shughuli zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed, alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, ufanisi wa uendeshaji pamoja na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema kati ya mwaka 2016 na 2020 Serikali ilipokea gawio la jumla la Shilingi bilioni 7.65, lakini katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 gawio hilo liliongezeka hadi Shilingi bilioni 30.65, ukuaji unaoonyesha mabadiliko makubwa ya utendaji wa kampuni hiyo.

Mohamed alisema gawio hilo ni sehemu ya faida inayorejeshwa kwa wanahisa baada ya kampuni kulipia gharama zake zote za uendeshaji, huku fedha zinazopelekwa Serikalini zikisaidia kugharamia utekelezaji wa bajeti ya Taifa na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, TIPER imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 105 kuboresha matangi ya kuhifadhi mafuta, mifumo ya usafirishaji, kuzima moto na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kutoka lita milioni 253 hadi milioni 313.

Aidha, alisema kuanza kutumika kwa mfumo wa Single Receiving Terminal (SRT) wa mafuta ya dizeli Januari 2025 kumeongeza ufanisi wa shughuli za bandari kwa kupunguza muda wa meli kupakua mafuta kutoka wastani wa siku tisa hadi siku nne, hatua iliyopunguza gharama za ucheleweshaji na kuongeza idadi ya meli zinazohudumiwa.

Mohamed alisema TIPER sasa imeandaa mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 265 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kusafirisha mafuta, hatua itakayoiwezesha Tanzania kuendelea kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika Afrika Mashariki na Kati.

Rais wa Jamhuri ya Muungwana wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan (katikati)akikabidhi Tuzo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tiper Balozi Mathias Chikawe(kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Tiper  Mohamed Mohamed (kulia) wakati wa hafla ya Siku ya Gawio ambapo TIPER imekabidhi gawio la Sh.Bilioni 15 kwa Rais Samia jana Juni 30,Ikulu jijini Dar es Salaam

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: