Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutege, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha ya Uandaaji wa Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Wakati wa Dharura kwa Huduma za Mifugo Tanzania, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agness K. Meena. Warsha hiyo imefanyika leo Juni 1, 2026, katika Ukumbi wa Masailand Hall jijini Arusha.

Mkurugenzi Msaidizi wa Epidemiolojia na Magonjwa ya Mifugo Yanayovuka Mipaka (TADs) akitoa mchango wake katika majadiliano ya Warsha ya Uandaaji wa Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Wakati wa Dharura kwa Huduma za Mifugo Tanzania, iliyofanyika leo Juni 1, 2026, jijini Arusha.

Afisa Habari II wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Chiku Makwai, akitoa mchango wake katika majadiliano ya Warsha ya Uandaaji wa Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Wakati wa Dharura kwa Huduma za Mifugo Tanzania, iliyofanyika leo Juni 1, 2026, jijini Arusha.

Afisa Sheria I wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Denis Ukaka, akitoa mchango wake katika majadiliano ya Warsha ya Uandaaji wa Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Wakati wa Dharura kwa Huduma za Mifugo Tanzania, iliyofanyika leo Juni 1, 2026, jijini Arusha.

Na Chiku Makwai – ARUSHA

Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limeanza mchakato wa kuandaa Rasimu ya Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano Wakati wa Dharura kwa Huduma za Mifugo Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya mifugo.

Warsha ya kuandaa rasimu hiyo imefunguliwa leo, Juni 1, 2026, katika Ukumbi wa Masailand Hall jijini Arusha na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dkt. Benezeth Lutege, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhe. Agness K. Meena.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Dkt. Lutege amesema mawasiliano yenye ufanisi ni nyenzo muhimu katika kudhibiti na kukabili milipuko ya magonjwa ya mifugo kwa kuwa huwezesha utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati kwa wadau wote wanaohusika.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari na mwitikio wa haraka ili kuhakikisha magonjwa ya mifugo yanagunduliwa na kudhibitiwa mapema kabla hayajasababisha athari kubwa kwa uzalishaji, biashara ya mifugo na afya ya jamii.

“Mkakati huu utaweka msingi wa kuwa na mfumo mmoja wa kitaifa wa mawasiliano ya dharura utakaoongoza utoaji wa taarifa, ushirikishwaji wa wadau na usimamizi wa mawasiliano wakati wa matukio ya milipuko ya magonjwa ya mifugo,” amesema Dkt. Lutege.

Aidha, amebainisha kuwa magonjwa mbalimbali ya mifugo, ikiwemo Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever), yanahitaji uratibu madhubuti wa mawasiliano ili kuhakikisha wananchi na wadau wanapata taarifa sahihi zitakazowawezesha kuchukua hatua stahiki kwa wakati.

Warsha hiyo imewakutanisha wataalamu wa mifugo, afya ya wanyama, mawasiliano na wadau wengine kutoka taasisi za Serikali pamoja na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kujadili mbinu bora za mawasiliano ya hatari, usimamizi wa taarifa za dharura na mikakati ya kuimarisha mwitikio wakati wa milipuko ya magonjwa.

Washiriki pia wanatarajiwa kujadili matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa taarifa pamoja na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya afya ya wanyama na afya ya binadamu kwa kuzingatia dhana ya Afya Moja (One Health).

Kupitia warsha hiyo, Tanzania inatarajia kuwa na mkakati madhubuti wa mawasiliano ya dharura utakaosaidia kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema, kuongeza mwitikio wa haraka wakati wa matukio ya dharura na kulinda ustawi wa mifugo sambamba na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: