Serikali imeendelea kuweka msukumo mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala nchini, hususan umeme na gesi asilia, katika sekta ya usafiri na matumizi ya majumbani, kupitia mapendekezo mapya ya hatua za kodi kwa mwaka wa fedha 2026/27.


Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya makadirio ya mapato na matumizi Bungeni, Waziri wa Fedha,Balozi Dkt Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kifedha na kodi zinazolenga kupunguza gharama za uwekezaji na kuongeza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Serikali imeendelea kutoa msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa magari yanayotumia umeme na gesi asilia kwa kuzingatia ukubwa wa injini, sambamba na msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) inayotumika kwenye magari.

Aidha, Serikali imeondoa VAT kwenye vifaa vinavyotumika katika miundombinu ya gesi asilia (CNG), ikiwemo compressors, vifaa vya kupimia, mitambo ya kuhifadhi gesi, magari maalum ya usafirishaji na pampu za kujazia gesi. Hatua hiyo pia inahusisha msamaha wa kodi katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa CNG pamoja na vifaa vinavyotumika kubadili magari kutoka mafuta ya petroli kwenda kwenye gesi au umeme.

Katika sekta ya uzalishaji wa ndani, Serikali imeweka pia msamaha wa VAT kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza mitungi ya gesi kwa matumizi ya majumbani na magari, pamoja na kutoa unafuu wa ushuru wa forodha kwa waunganishaji na wazalishaji wa vyombo vya moto vinavyotumia nishati safi nchini chini ya kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki za mwaka 2025.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Serikali inapendekeza hatua zaidi ikiwemo msamaha wa VAT kwa vifaa vya vituo vya kuchaji magari ya umeme (EV charging stations), pamoja na kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa magari yanayotumia umeme.

Pia, Serikali imependekeza msamaha wa VAT kwa mita janja za gesi ya kupikia (LPG smart meters) zitakazoingizwa nchini na kusambazwa na wasambazaji wa gesi pekee, sambamba na majadiliano ya kutoa unafuu wa kodi kwa waunganishaji wa magari ya umeme nchini ili kuchochea uzalishaji wa ndani.

Hatua hizo Serikali inasema, zinalenga kupunguza gharama za matumizi ya nishati safi, kuvutia uwekezaji katika sekta ya nishati mbadala, kuimarisha viwanda vya ndani, na hatimaye kulinda mazingira kupitia upunguzaji wa matumizi ya mafuta ya kisukuku.

Kwa ujumla, mkakati huu unaonekana kuwa sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kuhamia kwenye uchumi wa kijani unaotegemea nishati safi na endelevu nchini.

Share To:

Post A Comment: