Awataka kuwa na nidhamu na kusoma kwa bidii

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaasa wanafunzi walioshiriki mashindano ya UMISSETA mwaka 2026 kuendeleza vipaji vya michezo na Sanaa walivyonavyo kwani vitawasaidia katika maisha yao ya baadaye, huku akiwataka kuzingatia nidhamu na kusoma kwa bidii ili  kufikia ndoto zao na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa wanafunzi leo Juni 28, 2026 mjini Iringa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Lugalo, wakati akifunga mashindano ya UMISSETA kwa mwaka wa 2026.

“Nina wasihi muendelee kuwa na nidhamu, kujituma katika masomo yenu na kuendeleza vipaji vyenu vya michezo na sanaa, msiviache vipaji vyenu kwani hata mimi juzi tulipokuwa tunapokea Mwenge wa Uhuru Lushoto nilijikuta nikikumbushia kipaji changu cha kupiga ngoma za utamaduni na kuimba kwa umahiri,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amewahakikishia wanafunzi hao kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuhakikisha vipaji vya wanafunzi vinaibuliwa, vinatambuliwa, vinakuzwa ili kuwanufaisha na kulinufaisha taifa kupitia ushiriki wao katika kuliwakilisha taifa kwenye mashindano ya michezo na Sanaa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu, michezo, sanaa na maendeleo ya vijana kwenye ajenda kuu ya taifa na kuongeza kuwa, uwekezaji huo unaendelea kuweka msingi imara wa kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto na vijana wa Tanzania.

 Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Bw. Atupele Mwambene amesema kuwa, ushiriki wa wanafunzi katika michezo mbalimbali ya UMITASHUMTA na UMISSETA umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kitaifa la kuibua vipaji, kuimarisha afya, kujenga urafiki na kuendeleza umoja wa kitaifa miongoni mwa wanafunzi. 

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Leah Kihimbi amemuhakikishia Prof. Shemdoe kuwa wizara yake itatekeleza ipasavyo jukumu la kuibua kuendeleza vipaji na vipawa vinavyotokana na mashindano hayo ya sanaa na michezo shuleni. 

Mwakilishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ambaye ni Afisa Mdhamini Bw. Mohamed Nassoro Salimu amesema Zanzibar inakwenda kujipanga ili kuleta ushindani mkubwa katika mashindano ya mwakani, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kufanya mageuzi katika sekta ya michezo.

Akitoa neno la shukrani, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru amewashukuru maafisa elimu, wakuu wa shule, walimu, waratibu wa michezo na walezi wa wanafunzi, kwa kazi kubwa walioifanya ya kuwaandaa na kuwaleta wanafunzi katika mashindano ambayo yamewawezesha kujifunza thamani ya nidhamu, ushindani wa haki, uvumilivu, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.













Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
رسالة أقدم

Post A Comment: