NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mkutano wa kimataifa wa siku tatu wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere umezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kujadili masuala ya siasa za kimataifa (geopolitics), maendeleo na mwelekeo mpya wa Afrika katika mazingira ya dunia yanayobadilika kwa kasi.
Mkutano huo, unaofanyika kwa mara ya 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008, umewakutanisha wasomi, watafiti, watunga sera na viongozi mbalimbali kujadili nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa, hususan wakati wa ushindani wa mataifa makubwa pamoja na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayoendelea duniani.
Akizungumza baada ya kusimikwa rasmi kuwa Mwenyekiti mpya wa Kigoda hicho, Prof. Alexander Makulilo amesema Afrika inahitaji mshikamano wa dhati katika nyanja za kisiasa na kiuchumi ili kuimarisha nguvu yake ya pamoja na kuongeza ushawishi wake katika maamuzi ya kimataifa.
Amesema bila umoja wa kweli, nchi za Afrika zitaendelea kuwa katika nafasi dhaifu katika majukwaa ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika biashara, viwanda, sera za kikanda na uwekezaji wa pamoja ili kufanikisha maendeleo endelevu ya bara hilo.
Aidha, Profesa Makulilo amesisitiza umuhimu wa Afrika kujenga uwezo wa kuzalisha maarifa yake yenyewe badala ya kutegemea mataifa ya nje, akibainisha kuwa maendeleo ya kweli yatapatikana pale bara hilo litakapowekeza zaidi katika elimu, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara wa maarifa na kuongeza ushindani katika jukwaa la kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mstaafu wa Kigoda hicho, Prof. Issa Shivji, amesisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa kitaaluma katika taasisi za elimu ya juu kama msingi wa kukuza fikra huru, mjadala wa kisomi na uzalishaji wa maarifa mapya.
Profesa Shivji pia amehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda kupitia misingi ya Pan-Africanism, akieleza kuwa mshikamano wa bara la Afrika ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa, huku akionya kuwa ukosefu wa umoja utaendelea kulifanya bara hilo kubaki katika utegemezi wa kimataifa.




Post A Comment: