SERIKALI imezindua rasmi Mpango wa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Maafisa Elimu Kata nchini, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa uongozi wa shule, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mei 28, 2026 mkoani Mwanza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa viongozi wa elimu hususan wakuu wa shule za sekondari ambao kwa muda mrefu hawajapata mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa kiwango kinacholingana na mahitaji ya sasa ya mfumo wa elimu.

Amesema tofauti na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wamekuwa wakipata mafunzo ya uongozi, wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakikosa fursa hiyo kwa kipindi kirefu, hali iliyofanya Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha mpango huo wa kitaifa ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa elimu.

“Mpango huu ni fursa muhimu kwa viongozi wa shule kupata maarifa ya kisasa ya uongozi, utawala bora na usimamizi wa elimu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku,” alisema Prof. Nombo.

Prof. Nombo ameeleza kuwa mafunzo hayo hayatawahusu wakuu wa shule pekee, bali yatawajumuisha pia wakuu wasaidizi wa shule za sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha viongozi wote wa elimu wanakuwa na uelewa unaofanana katika kusimamia ubora wa elimu.

Aidha, amesema Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri watashiriki kama wasimamizi wa utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao, hatua itakayosaidia kuhakikisha maarifa yanayopatikana yanaenda sambamba na maboresho ya mifumo ya usimamizi wa elimu.

Pamoja na hayo ameipongeza ADEM pamoja na VVOB-Tanzania kwa kuandaa na kufadhili mpango huo, akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030, jumla ya viongozi wa elimu 16,000 wanatarajiwa kufikiwa, wakiwemo wakuu wa shule na wasaidizi wao 12,000 pamoja na Maafisa Elimu Kata 4,000.

Amesema mbali na mafunzo ya uongozi, mpango huo utatoa fursa za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kupitia scholarships, huku akiwataka viongozi wa elimu kuchangamkia nafasi hizo kwa kuwa elimu ni mchakato endelevu usio na kikomo.

Amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa miezi mitano kwa mfumo wa elimu masafa na ana kwa ana (blended learning), ambapo washiriki wataendelea kutekeleza majukumu yao ya kawaida huku wakijifunza na kutekeleza shughuli za kimradi zinazohusiana na usimamizi wa shule.

Amewataka viongozi wa elimu ngazi ya mkoa na halmashauri kutoa ushirikiano wa karibu kwa washiriki wa mafunzo ili kuwajengea mazingira rafiki ya kujifunza na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kikazi sambamba na mafunzo.

Aidha, amefafanua kuwa utekelezaji wa awamu ya kwanza utaanza mwezi Juni 2026 ukihusisha washiriki kutoka halmashauri 12 katika mikoa sita ya Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu na Shinyanga, huku kila mkoa ukianza na halmashauri mbili.

Katika mafunzo hayo, washiriki watajengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma yakiwemo uandaaji wa mipango mkakati, ufunzaji na uatamizi, uthibiti ubora wa ndani wa shule, uongozi wa ufundishaji na ujifunzaji, usimamizi wa mtaala ulioboreshwa wa mwaka 2023 pamoja na usimamizi wa mtaala unaojenga umahiri.

Wakati huo huo, Prof. Nombo amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa, ujenzi na ukarabati wa shule, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na uwekezaji katika elimu ya amali ili kuandaa wahitimu wenye maarifa, ujuzi na ushindani ifikapo mwaka 2050.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa wakuu wa shule za sekondari, hasa kutokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu kundi hilo halijapata mafunzo ya kina ya kiuongozi na kiutendaji.

Amesema kupitia mafunzo hayo, wakuu wa shule watapata maarifa na mbinu mpya zitakazowawezesha kusimamia shule kwa ufanisi zaidi, kujenga mazingira bora ya kujifunzia na hatimaye kuboresha matokeo ya wanafunzi.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wathibiti Ubora wa Shule, Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa elimu, jambo linalodhihirisha uzito na umuhimu unaowekwa katika kuimarisha uongozi wa elimu nchini.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: