Na OWM - TAMISEMI, Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Adolf Mkenda wamewapokea walimu wapatao 150 wa amali waliokwenda kwenye ziara ya mafunzo ya mwezi mmoja nchini India, ambayo yatawawezesha kutoa elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi nchini ili kukuza uchumi wa viwanda, kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, na kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la ajira.

Walimu hao mara baada ya kurejea nchini, walipata mwaliko wa Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kuhudhuria shughuli za Bunge Mei 04, 2026 jijini Dodoma na kupokelewa kwa pamoja na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Prof Shemdoe na Waziri wa Elimu Mhe. Prof. Mkenda ambao ofisi zao ziliratibu ziara ya mafunzo ya walimu hao  nchini India.

Akizunguza na walimu hao katika viwanja vya Bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 3 na kutoa kibali cha walimu hao kwenda kwenye ziara ya mafunzo nchini India ili kujifunza na kupata ujuzi utakaowawezesha kuleta athari chanya zaidi katika mfumo wa elimu ya ufundi.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka walimu hao kuhakikisha yote waliyojifunza nchini India wanaenda kuwafundisha wanafunzi madarasani na kwa vitendo ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuwa wabunifu, wajasiriamali na uwezo wa kushindana katika ajira za ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

“Vijana wetu wanahitaji kupata maarifa na ujuzi mlioupata kwenye ziara yenu ya mafunzo nchini India, hivyo nendeni mkawafundishe kwa umahiri ili waje kutoa mchango katika maendeleo ya taifa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali iliwapeleka walimu hao wapatao 150 nchini India kwenda kujifunza namna wanavyoendesha shule za amali na kutekeleza mtaala wao wa elimu ili wakirejea nchini waweze kuwa chachu ya kutekeleza vema mtaala mpya wa elimu kwa kutumia vema teknolojia iliyopo katika kuwafundisha vijana wa kitanzania elimu ya ufundi stadi.

“Sisi tulichukua walimu 150 na kuwapeleka India ili waende kujifunza namna masomo ya elimu ya amali yanavyofundishwa ili wakirejea waje kuwa chachu ya kuboresha namna ya kufundisha masomo ya amali, hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya mapema ya Mhe. Rais kwa wizara ya Elimu na yale aliyoyatoa wakati akizindua sera yetu ya elimu,” amesema Prof. Mkenda.

Share To:

Post A Comment: