NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Wahitimu 12 wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wamehitimu mafunzo ya awali ya lugha ya Kijapani, hatua inayolenga kuongeza ujuzi na ushindani wao katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Akizungumza Aprili 30, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Prosper Mgaya, amesema kuanzishwa kwa kozi hiyo ni mkakati wa chuo kuongeza uwezo wa wahitimu wake, hususan wahudumu wa ndege, ambao awali walikuwa wakitumia lugha mbili pekee—Kiswahili na Kiingereza.
Ameeleza kuwa NIT imepanga kupanua wigo wa mafunzo ya lugha kwa kuanzisha pia lugha ya Kichina na Kifaransa, ili kuwajengea wahitimu uwezo mpana zaidi wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Tulikuwa na wataalamu kutoka JICA ambao wameahidi kutusaidia kwa kutoa vifaa vitakavyosaidia katika ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kijapani kwa wanafunzi wetu,” amesema Mgaya.
Aidha, amesema chuo hicho kiko katika mazungumzo na Ubalozi wa China nchini kwa lengo la kuanzisha rasmi mafunzo ya lugha ya Kichina, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa na ujuzi wa lugha zaidi ya moja.
Mgaya ameongeza kuwa licha ya ongezeko kubwa la mwamko wa udahili, kwa sasa chuo kimeweka kipaumbele kwa wahudumu wa ndege ili kuwasaidia kukidhi ushindani uliopo katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mwalimu wa NIT, Sarah Frolence Masae, ambaye pia ni mmoja wa wahitimu wa kozi hiyo katika kundi la kwanza, amesema mafunzo hayo yatamwezesha kuboresha ufundishaji wake na kuongeza ufanisi kazini.
Naye Mhandisi Elton Mfinanga, mmoja wa wahitimu, amesema kozi hiyo haina masharti magumu ya elimu, hivyo kumpa nafasi mtu yeyote kujifunza. Ameongeza kuwa ujuzi huo utamsaidia kufanikisha ndoto yake ya kupata ufadhili wa masomo ya uzamivu nchini Japani

Post A Comment: