Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonesha nafasi yake katika kuchochea maendeleo ya viwanda na kukuza ubunifu wa vijana kwa kutoa elimu ya viwango na ubora wa bidhaa katika Maonesho ya Fursa za Kazi na Ubunifu kwa Vijana (Career Fair 2026), hatua inayolenga kuwajengea vijana uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika soko la ndani na kimataifa.

Maonesho hayo yaliyofanyika leo Mei 29, 2026 katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) chini ya kaulimbiu isemayo “Ubunifu na Ujuzi kwa Vijana ni Msingi wa Ukuaji wa Biashara na Viwanda Tanzania”, yaliwakutanisha wanafunzi, wahitimu wa zamani (Alumni), wabunifu na wadau mbalimbali wa maendeleo ya biashara na viwanda kwa lengo la kujadili fursa, maarifa na njia za kukuza uchumi wa viwanda kupitia vijana.

Mgeni rasmi wa maonesho hayo alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ambaye alitembelea mabanda mbalimbali na kujionea kazi za ubunifu zinazofanywa na vijana wa Kitanzania pamoja na juhudi za taasisi zinazosaidia kukuza mazingira bora ya uzalishaji na biashara.

Katika ushiriki wake, TBS ilitoa elimu kwa wanafunzi na wabunifu kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika bidhaa wanazozalisha, namna ya kutumia vipimo sahihi pamoja na taratibu za kupata Alama ya Ubora ya TBS, hatua inayotajwa kuwa nyenzo muhimu ya kuongeza uaminifu na ushindani wa bidhaa sokoni.

Akizungumza katika banda la TBS, Afisa Metrolojia wa TBS, Mhandisi Angela Charles, amesema vijana wengi nchini wana ubunifu mkubwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye tija, lakini bado wanahitaji mwongozo wa kitaalamu kuhusu viwango, vipimo sahihi na udhibiti wa ubora ili kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la kisasa.

Amesema ushiriki wa TBS katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuwafikia vijana moja kwa moja ili kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa ubora wa bidhaa, taratibu za upimaji na manufaa ya kupata ithibati ya viwango kwa bidhaa zao.

“Tunataka vijana waelewe kuwa ubunifu pekee hautoshi, bali ubora ndio unaoongeza thamani ya bidhaa na kuifanya iaminiwe zaidi sokoni,” amesema Mhandisi Angela.

Kwa upande wake, mmoja wa wabunifu walioshiriki maoneshoni hayo, Omary Kisoma ambaye anajihusisha na utengenezaji wa sabuni ya maji, amesema elimu aliyoipata kutoka TBS imemsaidia kuelewa hatua muhimu za kuboresha bidhaa yake na namna ya kupata Alama ya Ubora.

Amesema awali alikuwa akihofia kuwa mchakato wa kupata ithibati ungekuwa mgumu na wenye gharama kubwa, lakini baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa TBS ameona kuwa ni utaratibu unaowezekana na wenye mchango mkubwa katika kukuza biashara.

“Nimepata uelewa mkubwa kuhusu namna ya kuboresha bidhaa yangu na hatua za kupata alama ya ubora ili niweze kufikia masoko makubwa zaidi, ikiwemo ya nje ya nchi,” amesema Omary.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Career Fair CBE 2026 umeendelea kuonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kusaidia vijana wabunifu nchini kwa kuwapatia maarifa ya ubora na viwango, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea uzalishaji wa bidhaa bora na zenye ushindani wa kimataifa.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: