Serikali kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) imeendelea kuimarisha huduma za uhakiki wa vipimo nchini kwa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha Uhakiki kilichopo eneo la Misugusugu, mkoani Pwani, ambacho kimegharimu jumla ya shilingi bilioni 7.3.

Kituo hicho kilichojengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 2.4 ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kusogeza karibu huduma za vipimo kwa wananchi na wadau wa kibiashara, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kitaifa ya udhibiti wa ubora wa vipimo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa Bungeni, kituo hicho kitahusika na uhakiki wa vifaa mbalimbali vinavyotumika katika sekta za nishati na maji, ikiwemo matenki ya magari yanayosafirisha vimiminika, mita mpya za umeme pamoja na dira za maji kabla ya kufungwa kwa watumiaji.

Lengo kuu la uhakiki huo ni kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinakidhi viwango vilivyowekwa kitaifa na kimataifa, na hivyo kuhakikisha usahihi wa vipimo, kulinda haki za watumiaji na wauzaji, pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Hata hivyo, WMA imebainisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wake, ikiwemo mwitikio hafifu kutoka kwa baadhi ya wazabuni wa mita za umeme kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la kuwasilisha mita hizo kwa ajili ya uhakiki kabla ya kusambazwa kwa taasisi nunuzi.

Changamoto nyingine ni malimbikizo ya muda mrefu ya madai ya malipo ya huduma za uhakiki wa dira za maji kutoka kwa baadhi ya kampuni zilizopewa zabuni, hali inayoweza kuathiri uendelevu wa huduma na ufanisi wa taasisi hiyo.

Akizungumza Bungeni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile, amesema kamati yake imebaini hatua nzuri zilizofikiwa na WMA katika kuboresha huduma zake, ikiwemo ujenzi wa kituo hicho cha kisasa cha Misugusugu.

Ditopile amesema kuwa kamati imepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya uhakiki wa vipimo, lakini pia imesisitiza umuhimu wa kuongeza ufuatiliaji wa wazabuni ili kuhakikisha wanazingatia matakwa ya kisheria kabla ya kusambaza vifaa kwa wananchi.

Aidha, alibainisha kuwa changamoto ya malimbikizo ya madeni ya huduma za uhakiki inapaswa kushughulikiwa kwa haraka ili kuepusha athari katika uendeshaji wa taasisi na utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.

Kamati hiyo pia imeitaka Serikali kuendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya vipimo ili kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika nchini vinakuwa sahihi na vinakidhi viwango vilivyowekwa, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali za uchumi.

Kwa ujumla, ujenzi wa Kituo cha Misugusugu unatajwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya vipimo nchini, ukiwa na lengo la kuongeza uwazi, usahihi na ulinzi kwa watumiaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.


Share To:

Post A Comment: