Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa, zoezi la kubadilisha tahasusi na kozi za vyuo vya kati kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2025 limeanza rasmi leo Aprili 11, 2026 na litahitimishwa Mei 10, 2026.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Aprili 11, 2026 jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2025 kufanya mabadiliko ya Tahasusi za kidato cha tano na kozi za vyuo vya kati kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha tano na Vyuo mwaka 2026.
“Ninawahimiza wanafunzi, wazazi na walezi kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka wahitimu kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka wahitimu kuzingatia muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa, kwani mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko tahasusi na kozi.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, huduma ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na dawati la huduma la kwa mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kuwasiliana moja kwa moja na kituo cha huduma kwa wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210 na kuongeza kuwa, mwanafunzi, mzazi au mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri.

Post A Comment: