Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekutana na kuzungumza na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam Aprili 21, 2026.

Akizungumza katika kikao hicho,Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Millya (Mb.), amesema kikao hicho kimewapa Wabunge mwongozo wa jinsi wanavyopaswa kutekeleza majukumu yao na kutetea nafasi na sauti ya Tanzania ndani ya Bunge hilo la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Ninyi ni wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, ni wajibu wenu kuhakikisha sauti na nafasi ya Tanzania inaimarika kwa kutekeleza diplomasia ya uchumi kama Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania inavyosema”, alisema.

Mheshimiwa Millya alieleza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele kulipa michango yake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kikamilifu, na kusisitiza kuwa itaendelea kutimiza wajibu huo kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa malengo na dhamira ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Aliwaambia kuwa, Tanzania imejipanga kutumia nafasi ya Mtanzania Balozi Stephen Mbundi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maslahi mapana ya nchi.

Alisema kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa muongozo wa ushirikiano kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuimarisha utendaji wa wawakilishi wa Tanzania katika Vyombo vya kikanda na kimataifa.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, aliwaeleza wabunge hao kuwa mkutano huo unalenga kutoa dira na mwelekeo wa ushiriki wa Tanzania ndani ya bunge hilo la Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wizarani akiwasilisha mpango wa bajeti na sera ya mambo ya nje alisisitiza umuhimu wa Wabunge hao kuoanisha vipaumbele vya taifa na ajenda za kikanda na hivyo kuiletea nchi matokeo chanya.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Mikakati na Siasa za Kimataifa Wizarani Balozi Thobias Makoba, alibainisha haja ya Tanzania kuendelea kujiimarisha kimkakati katika ushiriki wake kidiplomasia duniani wakati ikiendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Ansar Kachwamba (Mb.), aliishukuru Wizara kwa kikao hicho ambacho kimewapa mwongozo wa kuangazia Maslahi ya nchi katika Bunge hilo na watafanyia kazi waliyotumwa na nchi kwa ukamilifu.

Naye Mhe. Dkt. Salema alisema kikao hicho kimewapa mwanga wa namna ambavyo Mbunge wa EALA anavyopaswa kuwa na kwamba italeta tija kwa nchi kwa kuwa sasa watakuwa na maono yanayofanana.
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: