

Na Oscar Assenga, Muheza
Mjumbe wa Kamati ya Hamasa Kanda ya Kaskazini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lukindo Mohamed, ametangaza rasmi kujiondoa ndani ya chama hicho na kueleza kuwa hatarajii kujiunga na chama kingine chochote cha siasa.
Lukindo, ambaye pia aliwahi kuwa Kaimu Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya ya Muheza, amesema amefikia uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe ili aweze kuwa huru na kujikita katika shughuli zake binafsi, ikiwemo kilimo na malezi ya familia.
Akizungumza na waandishi wa habari Lukindo alieleza kuwa moja ya sababu kubwa ya kujiondoa kwake ni kutoridhishwa na mwelekeo wa chama chake, hususan kuhimiza maandamano kama njia ya kutatua changamoto za kisiasa.
Alisema kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi ya kidemokrasia inayoruhusu wananchi kuchagua viongozi kwa kura bado kumekuwa na msisitizo wa mara kwa mara wa kufanya maandamano, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara kwa wananchi, ikiwemo majeruhi na vifo.
“Naamini kabisa kuwa suluhu ya matatizo ya nchi yetu haiwezi kupatikana kupitia maandamano, bali kupitia mazungumzo na maridhiano ni muhimu viongozi wa vyama vya siasa kukaa pamoja na kujadiliana kwa lengo la kuijenga nchi,” alisema Lukindo.
Aliongeza kuwa hajashawishiwa na mtu yeyote kuchukua uamuzi huo, bali ametumia busara na uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa, akieleza kuwa amehudumu ndani ya chama hicho tangu mwaka 1992 katika ngazi mbalimbali, ikiwemo Katibu wa Wilaya ya Muheza kuanzia mwaka 2010 hadi 2024.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Lushoto, Andrew Mjema, naye ametangaza kujiondoa ndani ya chama hicho, akieleza kuwa amechoshwa na kile alichokiita siasa za matamko na maandamano zisizo na tija kwa wanachama wa kawaida.
Mjema alisema kuwa mara nyingi viongozi wa juu wamekuwa wakitoa wito wa maandamano huku madhara yake yakiwakumba zaidi wanachama wa ngazi za chini, hali ambayo ameona si ya haki.
“Viongozi wanazungumza kuhusu maandamano lakini hawashiriki moja kwa moja, wanaoumia ni wanachama wa chini. Hii si sawa, ndiyo maana nimeamua kujiondoa na kuendelea na shughuli zangu za ufundi,” alisema Mjema.
Alisisitiza kuwa hatajiunga na chama chochote cha siasa, akiongeza kuwa anahitaji muda wa kujiendeleza kiuchumi na kuishi maisha yake binafsi nje ya siasa.
Wote wawili wamehitimisha kwa kushauri vyama vya siasa nchini kuweka mbele mazungumzo na maridhiano badala ya maandamano, wakiamini kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kudumisha amani na kuleta maendeleo nchini.

Post A Comment: