Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Moremi Marwa akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam uliofanyika leo Aprili 22, 2026 Jijini Dar es Salaam.
******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba yameelezwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ufanisi wa taasisi, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikichukua hatua za makusudi kuboresha huduma na utendaji kupitia mifumo ya kidijitali.
Akizungumza Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi wa UDSM, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Moremi Marwa, amesema katika zama za mabadiliko ya haraka, teknolojia ina nafasi kubwa katika kurahisisha kazi na kuongeza tija.
Amesema kuwa matumizi ya Akili Mnemba yanaweza kuboresha ubora wa huduma pamoja na kuimarisha maamuzi ya kitaasisi, huku akiwahimiza wafanyakazi wa chuo hicho kujifunza na kutumia teknolojia hizo katika majukumu yao ya kila siku.
“Teknolojia, hususan hii ya akili mnemba, ina nafasi kubwa katika kurahisisha kazi, kuongeza ubora wa huduma na kuboresha maamuzi ya kitaasisi. Hivyo nawapongeza na kuwahimiza wafanyakazi wote kujifunza na kutumia teknolojia hizi,” amesema Marwa.
Mbali na hilo, Marwa amesisitiza umuhimu wa uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga imani kwa jamii na wadau wa chuo.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, amesema chuo kimepata mafanikio katika maeneo manne muhimu, ikiwemo kuimarika kwa mifumo ya ndani, udhibiti wa kifedha, utambuzi wa watumishi na ustawi wa wanajumuia wa chuo.
Amebainisha kuwa katika kuimarisha nidhamu ya fedha, chuo kimepata hati safi za ukaguzi kwa miaka minne mfululizo, huku hoja za ukaguzi zikipungua kutoka 86 hadi 34.
Aidha, ameeleza kuwa chuo kinaendelea kunufaika na mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi (HEET), ambao umechangia kuboresha miundombinu ya kufundishia, utafiti na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.
Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Moremi Marwa akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam uliofanyika leo Aprili 22, 2026 Jijini Dar es Salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam uliofanyika leo Aprili 22, 2026 Jijini Dar es Salaam.

Post A Comment: