Na James Mwanamyoto - Tanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekabidhi hundi yenye thamani ya Bilioni 2.761 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyonufaika na mkopo wa asilimia 10, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan aliyoitoa kwa wananchi kuwa ataitekeleza ndani ya siku 100 za uongozi wake.

Prof. Shemdoe amekabidhi hundi hiyo leo Januari 05, 2026 kwa vikundi hivyo jijini Tanga katika Uwanja wa Tangamano, mara baada ya kukagua shughuli za wajasiriamali walionufaika na mikopo ya asilimia 10 mkoani Tanga.

“Leo tumetoa Bilioni 2.761 kwa vikundi vya halmashauri ya jiji la Tanga, Korogwe Mji,  Korogwe wilaya , Lushoto, na Pangani, ambazo zitanufaisha vikundi vya wanawake 155, vijana 71 na wenye ulemavu 19 ambapo jumla ya ajira 1,715 zimetengenezwa,” amefafanua Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe, Balozi Dkt. Batilda Burian, kwa kusimamia vema utoaji wa mikopo ya asilimia 10 pamoja na kuandaa maonesho ya shughuli za vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo, na kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa mingine kuandaa maonesho kama Mkoa wa Tanga ulivyofanya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema katika kutekeleza ahadi hiyo ya Mhe. Rais, kwa Tanga jiji pekee Prof. Shemdoe amekabidhi hundi ya Bilioni 2 kwa vikundi 137 ambapo wanufaika ni wananchi 686.

Naye mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo ya asilimia 10, Bi. Zainab Abdallah ambaye ni mlemavu amesema yeye na mwenzie Mariam Siafu wamenufaika na mikopo hiyo ambapo wameweza kununua bajaji nne (4), awamu ya kwanza walipata  Shilingi Milioni 17 zilizowawesha kununua bajaji mbili (2) na awamu ya pili walipata Milioni 22 zilizowawezesha kununua bajaji (2) nyingine na hatimaye wamefanikiwa kuajiri madereva wanne (4).

Share To:

Post A Comment: