Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

 

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima ameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuweka kumbukumbu za ardhi vizuri jambo alilolieleza kuwa linasaidia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 

‘’Mhe Waziri kwa kweli nitoe pongezi kwa wizara yako kwa kuwa na kumbukumbu nzuri za wamiliki wa ardhi jambo hili limetusaidia kama mkoa wa morogoro kutatua migogoro ya ardhi pale inapojitokeza’’ amesema Bw. Malima

 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi moja ya vipaumbele vyake ni katika mwaka wa fedha 2025/2026 ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na katika maeneo ya kimkakati.

 

Bw. Malima amesema hayo tarehe 12 Desemba 2025 ofisini kwake alipokutana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo aliyekuwa mkoani humo kwa ajili ya kuhudhuria mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO).

 

Amesema, migogoro ya ardhi katika mkoa wake wa Morogoro imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi kubwa za wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa ambapo imefanya kazi kubwa ya kufikia wananchi kupitia Kliniki ya Ardhi.

 

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo alimueleza mkuu wa mkoa wa Morogoro kuwa, wizara yake kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyopo inatatuliwa na hakuna migogoro mipya inayozalishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

 

‘’Nikuhakikishe RC sisi ndani ya wizara tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha migogoro iliyopo tunaimaliza lakini pia hakuna migogoro mipya inayozalishwa’’ amesema Mhe. Dkt Akwilapo.

 

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amezihimiza taasisi za umma kuhakikisha zinalinda maeneo yao ili kuepuka uvamizi alioueleza kuwa ndiyo unaochangia kwa kikubwa migogoro ya ardhi katika maeneo ya umma.

Share To:

Post A Comment: