Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikabidhi Tuzo maalumu Meneja Mkazi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Paul Atallah (wa pili kushoto), kwa niaba ya kampuni hiyo na Qatar Foundation kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kusaidia watu wenye uhitaji.
...............................
Na Dotto Mwaibale, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.
Hussein Ali Mwinyi ametoa Tuzo maalum kwa Kampuni ya Emirates Leisure Retail
Zanzibar na Qatar Foundation kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kusaidia
watu wenye uhitaji.
Dkt. Mwinyi alitoa tuzo hizo katika kilele cha Maadhimisho
ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu yaliyofanyika Desemba 4, 2025 kwenye Ukumbi wa
Dr. Shein – Tunguu, Chuo Kikuu cha SUZA, Mkoa wa Kusini Unguja tukio
lililohudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo, mashirika ya
kijamii, na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Zanzibar.
Akihutubia katika maadhimisho hayo Rais Mwinyi aliwataka
wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwawezesha watu wenye
ulemavu na alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ni yale yanayowahusisha watu
wote bila kuacha kundi lolote nyuma.
Aidha, Dkt. Mwinyi alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wadau na
wahisani kwa kujitolea kwao kuchangia maendeleo ya jamii zenye watu wenye
ulemavu na kueleza kuwa Serikali itayafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa
ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa kamili za kutimiza malengo
yao.
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Paul Atallah, alilishukuru Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kwa kutambua mchango wa Emirates Leisure Retail na kueleza kwamba kampuni hiyo itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Serikali na jamii katika kuleta maendeleo chanya kwa watu wenye ulemavu.
Utambuzi wa Wadau Maalumu
Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar,
Ussi Khamis Debe, akizungumza kwenye maadhimisho hayo alitoa shukrani kwa wadau wote wanaounga mkono
juhudi za Serikali katika kusaidia watu wenye ulemavu.
Aidha, kwa nafasi ya kipekee alimshukuru Afisa Utawala Msaidizi wa Kampuni ya Emirates
Leisure Retail Zanzibar, Ramadhan Hussein Layya (Maarufu Msokolo),kwa
mchango wake mkubwa na wa muda mrefu, hususan katika kusaidia watu wenye
ulemavu wa ngozi kupitia misaada, ushiriki, na michango inayobadilisha maisha
ya wanufaika.
Kaulimbiu ya Maadhimisho:
"Uwezeshaji na Ushirikishwaji wa Watu Wenye Ulemavu kwa
Maendeleo Jumuishi."
Misaada Iliyotolewa katika maadhimisho hayo kwa ajili ya
makundi mbalimbali ya wahitaji ni
Vyerehani kwa ajili ya kujiajiri, kofia maalumu (round hats)
kwa ulinzi wa ngozi, miwani ya kinga na vifaa vya kurekebisha uoni, baiskeli za
mwendo kwa watu wenye ulemavu wa viungo, fedha za mikopo kwa kuanzisha au
kuendeleza biashara.
Vifaa vingine vilivyotolewa ni vya kuongeza uwezo wa kujitegemea
mashine za kusaga nafaka.
Misaada hiyo imeleta furaha, matumaini, na thamani kubwa kwa
wanufaika na familia zao, ambayo inakwenda kuwasaidia kutimiza ndoto zao na
kuimarisha ustawi wa familia zenye watu wenye uhitaji maalumu.
Kauli ya Emirates Leisure Retail Zanzibar na Qatar
Foundation:
Uongozi wa kampuni hizo umeeleza dhamira zao za kuendelea
kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha watu wenye ulemavu
Zanzibar wanapata fursa sawa za ustawi na maendeleo, na kuendelea kuwekeza katika
miradi ya kijamii inayobadilisha maisha ya watu wenye uhitaji maalumu.
Viongozi wa Kampuni hizo na wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.


Post A Comment: