_Kanali Sawala aagiza kasi na ubora katika utekelezaji wake_
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala amemuagiza Mkandarasi M/s Serengeti Limited anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Mradi wa uendelezaji Miji Tanzania TACTIC katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa Mkataba ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu hiyo inayotekelezwa Mkoani humo.
Kanali Sawala ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mradi huo unaohusisha uboreshaji wa miundombinu ya barabara za Chuno na Samia City, mitaro ya kutiririsha maji ya Mvua eneo la Kiyangu, ujenzi wa Kituo kikuu cha mabasi eneo la Chipuputa, Kituo cha wajasiriamali eneo la Skoya pamoja na jengo la usimamizi, mradi utakaogharimu jumla ya shilingi Bilioni 27. 49.
"”Ni matarajio yetu sote kuwa miradi hii italeta mabadiliko chanya kwa Wananchi wa Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani na wageni ambao watafaidi huduma za mahitaji mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, pamoja na mazingira bora ya shughuli za kiuchumi kwani ni dhahiri kuwa thamani ya maeneo husika itapanda na hivyo kusababisha ongezeko la mapato kwa Halmashauri yetu,” alisema Mhe. Kanali Sawala.
Kanali Sawala pia ametoa rai kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo inayojengwa kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda uliotarajiwa, akiielekeza Manispaa ya Mtwara kufanya tathmini ya miradi yenye kujiendesha ili kuhakikisha inakuwa chachu katika kuongeza mapato kwa Serikali na kuboresha huduma kuwa rafiki zaidi kwa wote.
“Mtu yeyote atakayetaka kuturudisha nyuma huyo tusikubaliana naye, miradi hii mbali na kuboresha huduma inaenda kuzalisha ajira kwa vijana wetu. Hivyo nikuombe mkandarasi kazi zote zinazoweza kufanywa na wazawa, wananchi wa marneo inapopita miradi wapewe kipaumbele ili pia wawe walinzi wa miradi hii,”alisema Kanali Sawala.
Aidha alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na TARURA kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Manyanga, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye ni Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, amesema mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Mtwara Mikindani na Miji mingine nchini ukiongeza fursa za ajira na uchumi kwa wananchi kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji na hivyo kuchangia maendeleo ya muda mfupi na mrefu katika Halmashauri hiyo.
Post A Comment: