Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ya chama chake itaendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya barabara, elimu na afya katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, iwapo wananchi watakiamini tena kuongoza nchi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
Akihutubia wananchi wa Korogwe leo, Dkt. Samia amesema CCM imeweka mpango wa kujenga barabara kuu mbili kwa kiwango cha lami zenye urefu wa zaidi ya kilomita 200. “Tutajenga barabara ya Soni – Bumbuli – Dindira – Korogwe yenye urefu wa kilomita 74 na pia barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Mabokweni yenye urefu wa kilomita 127.69,” alisema.
Ameongeza kuwa serikali pia itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege kwenye barabara ya Msambiazi – Lutindi – Kwabuluu ili kurahisisha usafiri na biashara ndani ya wilaya.
Kuhusu sekta ya elimu, Dkt. Samia amesema CCM imedhamiria kujenga madarasa 560 Korogwe, hatua itakayopunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa elimu bora.
Katika sekta ya afya, amesisitiza kuwa miradi ya kuboresha zahanati na vituo vya afya itaendelea kutekelezwa ili wananchi wa Korogwe wapate huduma bora karibu na makazi yao.
Post A Comment: