Na Denis Chambi, Tanga.
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuinadi sera ya chama hicho kwa siku tatu mkoani Tanga ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Madiwani ,wabunge na Rais unaotarajiwa kufanyika October 29,2025.
Akitoa taarifa hiyo kwa wananchi kupitia vyombo vya habari Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajab Abdulrahman amesema kuwa Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye atawasili mkoani hapa September 28 atafanya kampeni zake katika wilaya za Handeni, Pangani, Muheza , Korogwe na Tanga mjini katika mikutano ya hadharaakiwakaribisha wananchi kujitokeza kusikiliza sera ya chama hicho.
Rajabu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (MCC) ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa 2025 Mkoa wa Tanga umepata bahati ya kipekee ambapo Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya ziara mara mbili moja ikiwa ni ya kikazi ambapo amefungua miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
"Tunao ujio wa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chetu chama cha Mapinduzi (CCM) ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ataingia kwenye Mkoa wetu wa Tanga na tutampokea pale Mkata kwenye wilaya ya Handeni na atapata fursa ya kuwasalimia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo baadaye Moja kwa moja atakuja Tanga mjini kwa mapumziko."
"Siku ya pili tutaanzia kwenye wilaya ya Pangani kwa mkutano wa hadhara na baadaye Tanga mjini nichukue nafasi hii kuwaalika wananchi wanaoishi Mkoa wa Tanga kuja kumlaki" amesema Rajabu
"Sisi wananchi wa Tanga tunajiona ni watu wenye bahati kwa kupata ugeni huu mkubwa kwa mara ya pili ndani ya mwaka mmoja , alikuja kwa ziara ya kikazi miezi michache iliyopita na tunamshukuru alipokuja mambo ya kimaendeleo hususani miradi ile ambayo ilikuwa ikisuasua imeweza kukwamuka na sasa mambo yanaenda vizuri" amesema Mwenyekiti huyo.
Ameongeza kwa kusema kuwa chama hicho kimejipambanua katika kuwaletea wananchi maendeleo ambapo kupitia sera zake za mwaka 2025 zimegusa sekta zote zikiwemo za kimkakati.
" Wananchi tunaoishi kwenye Mkoa wa Tanga tutegemee maendeleo zaidi kwa sababu Dkt Samia ndiye mgombea pekee ambaye aliahidi kupitia ilani ya chama chetu na akatekeleza kwahiyo tunakwenda kuendelea tunaamini wananchi watakiunga mkono chama chetu na watampa kura nyingi za Urais Mgombea wetu kwa sababu amejipambanua katika kulinda amani ya nchi yetu lakini na katika miradi ya maendeleo" amesema Rajabu.
Post A Comment: