MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Joseph Isack maarufu kwa jina la Kadogoo, ameweka wazi siri ya mafanikio yake ya kisiasa kwa kumshukuru Hayati Edward Lowassa, akisema ndiye aliyemtabiria kuwa siku moja atakuwa Mbunge wa jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni yake uliofanyika katika eneo la Esilaley, Mji wa Kigongoni, wilayani Monduli, Kadogoo alisema anatamka kauli hiyo kutoka sakafuni mwa moyo wake, kwani Lowassa ndiye aliyemlea kisiasa na kumpa dira ya maisha ya uongozi.
“Sisi wana Monduli, hasa wanasiasa, hatuwezi kumzungumzia Lowassa kama mtu wa kawaida. Mimi ni zao lake. Yeye ndiye alinitabiria kuwa ipo siku nitakuwa Mbunge wa Monduli. Nikiwa hapa leo, naomba nimtaje hadharani, kwa sababu matunda haya ninayoyaona yametokana na mikono yake,” alisema Kadogoo huku akishangiliwa na umati.
Aliongeza kuwa Hayati Lowassa atabaki kuwa nguzo ya kisiasa ya Monduli na ataendelea kukumbukwa na viongozi mbalimbali aliowahi kuwajenga, kuanzia madiwani, viongozi wa wilaya, mkoa hadi Taifa.
Kadogoo alisema akipata nafasi ya kuliongoza jimbo hilo, atahakikisha anasimama kidete kuendeleza misingi ya maendeleo ambayo Lowassa aliyaacha na kuwaletea heshima wananchi wa Monduli.
Post A Comment: