VIJANA WATAWEZESHWA KUSOMA VETA BURE- DKT. SAMIA

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uwezeshaji wa vijana kwa elimu, ujuzi na ajira ni kipaumbele cha serikali yake katika miaka mitano ijayo, ikiwa ni sehemu ya kujenga taifa imara na lenye maendeleo ya watu.

Akihutubia leo Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Vwawa mkoani Songwe, Dkt. Samia amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye vyuo vya ufundi stadi (VETA) ili vijana wapate mafunzo yatakayowawezesha kuingia kwenye ajira na kujitegemea kiuchumi.

“Vijana wakimaliza VETA wanapata ujuzi wa moja kwa moja. Malipo ni kwa serikali, vijana hawalipi. Kama tunavyolipia shule ya msingi hadi sekondari, ndivyo tunavyolipia pia VETA, na wanaingia kwenye mpango wa mikopo ya wanafunzi,” amesema Dkt. Samia.

Dkt. Samia aliongeza kuwa, mbali na elimu, serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma za nishati safi ya kupikia ili wanawake na vijana wapate fursa za biashara na ajira katika sekta hiyo.

Aidha, amesema miradi mikubwa ya umeme kama ule wa kusafirisha nishati kutoka Iringa hadi Songwe kwa kilovoti 730 itafungua fursa za viwanda na ajira kwa vijana wa maeneo hayo.

Dkt. Samia amesisitiza kuwa vijana wa Tanzania ndio msingi wa maendeleo ya taifa, na serikali ya CCM imeweka mikakati ya kuhakikisha wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi mpya wa viwanda, kilimo cha kisasa na biashara.

Share To:

Post A Comment: