DKT. SAMIA AAHIDI KUENDELEZA RUZUKU YA MBOLEA SONGWE

Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa ruzuku akibainisha kuwa mbolea ya ruzuku tayari imewasili nchini na ipo katika hatua za kusambazwa kwa wakulima.

Akizungumza leo Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika, Vwawa, mkoani Songwe, Dkt. Samia amesema “Nimeongea na Waziri, ameniambia mbolea imeshaingia, bado kusambazwa. Mbolea ya kupandia tumbaku na ya mazao mengine tayari ipo. Kwa hiyo mbolea ya ruzuku itaendelea, ipo, bado kusambazwa lakini ipo”.

Dkt. Samia amewapongeza wakulima kwa jitihada zao, akibainisha kuwa mwaka huu Tanzania imeshika nafasi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa mahindi baada ya kuzalisha tani milioni 10. Kwa ujumla, amesema, Tanzania ina utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128.

“Hii inatupa faraja kwamba yale tunayotoa kwa ruzuku kama mbolea, mbegu na viuatilifu yanatumika vizuri, na wakulima wanazalisha kwa wingi sana,” amesema.

Akizungumzia miundombinu, Dkt. Samia amesema katika miaka mitano ijayo serikali itaendelea kujenga barabara na madaraja kwa lengo la kuhakikisha wilaya zote nchini zinaunganishwa na makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami.

“Madaraja yote pamoja na barabara, miaka mitano inayokuja tunakwenda kujenga. Lengo letu ni kuunganisha wilaya zote na makao makuu ya mkoa wa Songwe kwa barabara za lami. Hii kazi inaendelea na tutaifanya mpaka tuhakikishe wilaya zote Tanzania zimeunganishwa kwa lami,” amesema.

Share To:

Post A Comment: